HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 28, 2018

AGIZO LA WAZIRI UMMY MWALIMU LAANZA KUTEKELEZWA

Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Agizo alililotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu la kuanzishwa kwa madawati ya kijinsia katika shule za Msingi na Sekondari nchini alilotoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike Novemba 2017 Mkoani Mara limeanza utekelezaji wake.

Utekelezwaji wa agizo hilo umeanza kwa kuanzishwa kwa Programu ya kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi wa shule za Sekondari katika kukabiliana na  ukatili shuleni ambapo ndipo vitendo vingi vya ukatili ufanyika.

Programu hiyo iliyoanzishwa na Shirika la World Education na kuishirikisha Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yenye lengo la kuwajenga uwezo watendaji wanatekeleza afua za ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto kuwa na mbinu za kuzuia, kuchukua hatua na kushughulikia wahanga wa ukatili shuleni.

Akifungua kikao baina ya Wizara na Shirika la World Education kujadili Programu hiyo jijini Dodoma, Kaimu Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Marcel Katemba amesema kuwa Programu hiyo itasaidia kwa asilimia kubwa  kuweka mazingira salama na rafiki kwa watoto kusoma bila kusumbuliwa na  aina yoyote ya ukatili shuleni.

Ameongeza kuwa kupitia vitini vilivyopo katika Programu hiyo vitasaidia kuongeza weledi wa walimu kwa kubadili mitazamo na tabia zao na kuwa zenye nia ya kupinga vita ukatili na kuwa tayari kushughulikia vitendo vya ukatili punde vinapotokea.

“Matokeo ya ukatili nyumbani na shuleni unasababisha watoto wengi kuacha shule na wengine kukimbilia mitaani na hivyo kusababisha familia kukosa msaada hivyo kuwa tegemezi na hatimaye kusababisha kuendelea kwa mnyororo wa umasikini kuanzia ngazi ya familia hadi taifa” alisisitiza Bw. Katemba.

Aidha Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto Margareth Mussai amesema kuwa ukatili kwa watoto una athari kubwa kwa watoto wakiwa wadogo na wanapokuwa watu wazima kwa kujiingiza kwenye makundi yenye vitendo hatarishi katika jamii kwa kuongeza matukio ya uvunjifu wa amani na hata anapokuwa na familia ni rahisi kwa mtu huyo kuwa na tabia zisizofaa kwenye familia na jamii.

Margareth ameongeza kuwa kwa kuzingatia hilo Serikali na wadau wameona kuwa kuna haja ya kulishughulikia tatizo hili la ukatili katika hatua ya awali kuzuia matokeo mabaya ya muda mrefu kwa kutumia Programu hii kuwajengea uwezo watoa huduma za afya na maafisa Ustawi wa Jamii.

Kwa upande wake Mtaalamu wa masuala ya Elimu kutoka Shirika la World Education Bi. Grace Muro amesema kuwa taarifa ya hali ya ukatili kwa watoto ya mwaka 2011 inaonesha kuwa msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7 walifanyiwa ukatili wa kingono kabla hawajafikisha miaka 18. Taarifa za watoto  wengi  wanaofanyiwa vitendo vya ukatili haziripotiwi  na ni watoto wachache sana kati ya hao wanapata huduma mara baada ya kutokewa na vitendo vya ukatili wa aina hiyo pia taarifa hiyo inaonesha asilimia 72 ya wasichana na asilimia 71 ya wavulana wamefanyiwa ukatili wa kimwili na robo ya watoto nchini walifanyiwa ukatili wa kiakili.

Grace amesisitiza kuwa Programu hii ya kuwajengea uwezo waalimu na wanafunzi wa shule za Sekondari kupambana na ukatili shuleni itasaidia sana kuondokana na vitendo hivyo nchini.

Programu hii imezingatia ushirikishaji wa nyaraka mbalimbali za Kimataifa, Kanda na Serikali ikiwemo Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Mtoto, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sera, Mipango na Miongozo ya Serikali.
 Kaimu Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Marcel Katemba akifungua kikao baina ya Wizara na Shirika la World Education kujadili Programu ya kuwajengea uwezo waalimu na wanafunzi wa shule za Sekondari kupambana na ukatili shuleni kilichofanyika Jijini Dodoma.
 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Margareth Mussai akielezea jinsi ukatili kwa watoto unavyoleta  athari kubwa kwa watoto wakiwa wadogo na wanapokuwa watu wazima katika kikao baina ya Wizara na Shirika la World Education kujadili Programu ya kuwajengea uwezo waalimu na wanafunzi wa shule za Sekondari kupambana na ukatili shuleni kilichofanyika Jijini Dodoma.
 Mtaalamu wa masuala ya Elimu kutoka Shirika la World Education, Grace Muro akitoa taarifa ya hali ya ukatili kwa watoto ya mwaka 2011 ikionesha kuwa msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7 walifanyiwa ukatili wa kingono kabla hawajafikisha miaka 18 katika kikao baina ya Wizara na Shirika la World Education kujadili Programu ya kuwajengea uwezo waalimu na wanafunzi wa shule za Sekondari kupambana na ukatili shuleni kilichofanyika Jijini Dodoma.
 Mwakilishi Mkazi wa Shirika la World Education Tanzania, Lilian Badu akielezea dhumuni la Shirika lake kutekeleza Programu ya kuwajengea uwezo waalimu na wanafunzi wa shule za Sekondari kupambana na ukatili shuleni katika kikao kati ya Serikali na Shirika hilo kujadili Programu hiyo kilichofanyika Jijini Dodoma.
 Mtaalamu wa Masuala ya Kijinsia kutoka Shirika la Plan International Tanzania Dkt. Katanta Simwanzi akielezea masuala mbalimbali ya ukatili wa kijinsia na jinsi uanvyoleta madhara kwa jamii katika kikao baina ya Wizara na Shirika la World Education kujadili Programu ya kuwajengea uwezo waalimu na wanafunzi wa shule za Sekondari kupambana na ukatili shuleni kilichofanyika Jijini Dodoma.
 Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wadau kutoka Shirika la World Education wakijadilaina kuhusu utekelzaji wa Programu ya kuwajengea uwezo waalimu na wanafunzi wa shule za Sekondari kupambana na ukatili shuleni katika kikao kilichofanyika Jijini Dodoma. Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad