HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 9, 2018

Serikali Kuendelea Kuhakikisha Kuwa Pembejeo Zinawafikia Wakulima kwa Wakati

Frank Mvungi- MAELEZO
Serikali imesema itaendelea Kuhakikisha kuwa Pembejeo za Kilimo zinawafikia Wakulima kwa wakati na kwa bei nafuu ili kukuza sekta ya Kilimo.

Akijibu swali la Mbunge wa Mpanda Mjini Mhe. Sebastian Simon Kapufi, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa amesema kuwa ili kutimiza azma yakuwafikishia wakulima pembejeo kwa wakati Serikali inaratibu mahitaji, upatikanaji na matumizi yake na kuelekeza aina za pembejeo zinazofaa kwa kuzingatia msimu wa kilimo katika eneo husika.

“Serikali imeanzisha na kutumia mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha mbolea inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati,” alisisistiza Dkt. Mwanjelwa.
Akifafanua Mhe. Dkt. Mwanjwelwa amesema kuwa mfumo huo una faida nyingi ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa mbolea kutoka tani zaidi ya laki mbili hadi tani zaidi ya laki tatu kufikia mwezi Aprili 2018 na kupungua kwa bei za mbolea kwa kati ya asilimia 11 hadi 39.5 ikilinganishwa na bei ya mbolea kabla ya kuanza kwa mfumo huo.
"Tayari mbolea tani zaidi ya laki moja ikiwemo mbolea ya kupandia (DAP) tani zaidi ya elfu hamsini na tano na mbolea ya kukuzia (UREA) tani elfu hamsini na nne zimeingizwa na kusambazwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini ambapo mbolea hizo hutumika kwa zaidi ya asilimia 62 kwa mwaka," alisema Dkt. Mwanjelwa.
Kwa upande wa mbegu bora kuanzia mwaka 2017/2018 Serikali imefuta tozo (7) kwenye mbegu, ambapo mpango huu umelenga kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza upatikanaji na kupunguza bei ya mbegu bora kwa mkulima.
Aidha, Kwa kufutwa kwa tozo hizo Serikali inategemea bei ya mbegu bora itapungua na wakulima wengi wataweza kununua na kutumia ili kukuza kilimo hapa nchini na kuongeza uzalishaji.
Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikisisitiza uzalishaji wenye tija ili kukuza sekta ya viwanda hapa nchini na kuongeza ajira kwa wananchi hali itakayokuza pato la Taifa na uchumi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad