HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 10, 2018

BODI YA MIKOPO ELIMU YA JUU KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI WAPYA 40,000

*Maombi yote kupokelewa kwa njia ya mtandao, mkurugenzi ataja vipaumbele 
*Wenye ulemavu, yatima kupewa kipaumbele, RITA nao kuhakiki cheti cha kuzaliwa

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu(HESLB) imesema mwaka wa masomo wa 2018/2019 wamejipanga kutoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi wapya 40,000 na wanaoendelea zaidi ya 80,000 huku ikitangaza rasmi kuanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa muda wa miezi miwili na maombi yote yatapokelewa kwa njia ya mtandao.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Abdul -Razaq Badru wakati anatangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa miezi miwili na kufafanua jumla ya Sh.bilioni 427 zimetengwa.

Kuhusu maombi ya mkopo, Badru amesema leo wametangaza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya juu na maombi yote yawe kwa njia ya mtandao.

Amesema maombi hayo yatatumwa kupitia www.olas.heslb.go.tz na ni kuanzia leo hadi Julai 15 mwaka huu ili kuwapa fursa wanafunzi wahitaji kuwasilisha maombi hayo.

"Mwaka jana tulitoa mwezi mmoja,mwaka huu tumetoa muda wa zaidi ili kuwawezesha kusoma mwongozo kwa makini na kuzingatia maelekezo tunayopewa,"amesema Badru.

Amefafanua kuwa mwongozo huo kuna mambo muhimu yakiwamo ya sifa na taratibu za utoaji mikopo kwa mwaka 2018/2019.Mwongozo huo unapatikana katika lugha ya Kiswahili na Kingereza kwenye tovuti ya www.heslb.go.tz.

Amesema mambo muhimu yaliyomo kwenye mwongozo  ni kwamba kipaumbele kitatolewa kwa Watanzania wahitaji wanaosoma kozi zenye uhitaji mkubwa zaidi  kitaifa kama walimu wa masomo ya sayansi na hisabati, na sayansi ya afya ya binadamu.

Amesisitiza watatoa kipaumbele pia kwa wahitaji ambao ni yatima na wana nakala za vyeti vya vifo vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili na Udhamini (RITA) nao watapewa kipaumbele bila kujali kozi wanazosoma. Pia wengine watakaopewa kipaumbele ni waombaji wenye ulemavu uliothibitishwa na Mganga wa Mkoa au wilaya.

"Na waombaji mikopo ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya stashahada (diploma) au sekondari wana barua za uthibitisho kutoka taasisi zilizowadhali,"amesema Badru.

Kuhusu uboreshaji wa mfumo wa Tehama Badru amesema bodi ya mikopo kwa kushiikiana na kitengo cha kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waaendelea na maboresho makubwa ili kuifanya mifumo ya utoaji na urejeshaji mikopo kuwa rafiki zaidi kwa wateja.Kazi hiyo inatarajia kumalizika Agosti mwaka huu.

Badru ameeleza ni kwa mara ya kwanza bodi imetoa mwongozo wake wa uombaji mikopo katika lugha ya Kiswahili pamoja na kitabu chenye maswali  na majibu 21 kuhusu sifa na utaratibu wa kuwasilisha maombi ya mikopo.

Kwa upande wa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu RITA Emmy Hudson amesema waombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka huu mchakato wa uhakiki wa vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya vifo vya wazazi wa waombaji nchi zima wamekubaliana na bodi ya mikopo kutumia njia kadhaa ikiwamo mwombaji kuwasilisha nakala ya cheti katika ofisi ya mkuu wa wilaya alikokipata cheti cha kuzaliwa.

Pia waombaji wanaoishi nje ya wilaya walikopata cheti cha kuzaliwa pamoja na waliopo mkoa wa Dar es Salaam waingie katika mtandao kwa anuani http//uhakiki.rita.go.tz ili kupata maelezo ya jinsi ya kutuma nakala ya cheti na risiti ya malipo.

Hudso amesema ada ya uhakiki kwa kila cheti ni Sh.3000 ambayo inatakiwa kulipwa kupitia benki ya NMB kwenye akaunti ya Administrator General Collection Na 20610009881 au benki ya CRDB kwenye akaunti ya Administrator General Collection Account Na 0150339892600.
Mkurugenzi Mtendahi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul -Razaq Badru (kulia) akizungumza kwenye mkutano na wanahabari kuhusu kutangaza rasmi kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019 leo Alhamisi, Mei 10, 2018 jijini Dar es salaam. Katikati ni Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Hassan Mwang'ombe na kushoto Meneja Usajili wa RITA, Patricia Mpuya. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad