HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 10 May 2018

BARAZA LA WAFANYAKAZI TAASISI YA ELIMU YA WATU WAZMA LAKUTANA, MWENYEKITI WAO DK. NIHUKA AZUNGUMZIA MAFANIKIO NA CHANGAMOTO

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
MWENYEKITI wa Baraza la Wafanyakazi wa Tasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dk.Kassim Nihuka amesema pamoja na mafanikio ambayo imeyapata taasisi hiyo bado wangepata mafaniko makubwa zaidi iwapo changamoto zinazowakabili ikiwamo ya uhaba wa watumishi pamoja na miundombinu ingekuwa imepata ufumbuzi wake huku akifafanua tayari wameweka mikakati ya kuhakikisha wanaondoa changamoto hizo.

Dk. Nihuka ametoa kauli wakati anazungumza kwenye Mkutano wa Tisa wa Baraza la Wafanyakazi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima uliofanyika leo ambapo mgeni rasmi katika mkutano huo alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Theresia Mbando.

Akizungumza kwenye hotuba yake kwa mgeni rasmi ,Dk.Nihuka amesema mafanikio hayo huenda yangekuwa makubwa na mengi zaidi kama siyo changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwamo za ukosefu wa ofisi za kudumu  katika baadhi ya mikoa, upungufu wa wafanyakazi kutokana na kustaafu na vifo pamoja na
upungufu wa fedha za ndani.

Pia amesema ili kuendana na na msimamo wa Serikali wa Awamu ya Tano ,Menejimenti ya taasisi hiyo imedhamiria kuimarisha ukusanyaji wa mapato pamoja na kuhakikisha yanaenaelekezwa  katika kutekeleza malengo ya kipaumbele  kadiri ya mpango kazi wa taasisi na ule wa vituo,kampasi,idara na vitengo kwa ujumla.

"Katika kutekeleza hili wakufunzi wakazi, wakuu wa kampasi na mkuu wa idara ya mafunzo yanaagizwa kusimamia ukusanyaji wa ada kwa umakini mkubwa pamoja na kuhakikisha wanafunzi wale tu waliolipa ada ndio wanasajiliwa na kupata huduma katika vituo vyote,"amesema Dk.Nihuka.

Amefafanua taasisi inafanya tathimini ya mpango mkakati wa sasa(2014/2025-2018/2019) kwa lengo la kudurusu ili uendane na mahitaji ya sasa ya kujenga Tanzania ya uchumi wa kati inayotegemea  uchumiwa viwanda huku akisisitiza wanaendelea kutumia mpango mkakati uliopo  hadi hapo watakapokamilisha kudurusu na kupata mpango mkakati mpya.

Hivyo amesema matarajio yake wakuu wa idara na vitengo ,wakufunzi wakazi na wakuu wa kampasi wataendelea kuandaa mpango kazi na kutekeleza majukumu yao kwa kutumia mpango mkakati wa sasa.

Kuhusu mkutano huo, amesema ni mkutano wa tisa wa baraza la wafanyakazi wa taasisi hiyo na kueleza  baraza la wafanyakazi ni hitajio muhimu la kisheria linalolenga kuwashirikisha  wafanyakazi katika ushauri na usimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya taasisi ili kuhakikisha kuwa menejimenti na wafanyakazi wanatambua wajibu na haki pamoja na kuzingatia maadili ya utumishi.

"Menejimenti ya TEWW itaendelea kudumisha mikutano ya baraza la wafanyakazi ili kuongeza ushirikishwaji  wa wafanyakazi katika kutekeleza majukumu yetu kwa ustawi wa Taasisi na wafanyakazi kwa ujumla,"amesema.

Wakati huohuo amesema ili kuunga mkono  juhudi za Serikali  katika kuinua stadi za kisomo nchini, Taasisi hio imekamilisha mkakati wa kitaifa wa kisomo na elimu kwa umma utakaoanza kutekelezwa kuanzia Julai mwaka huu na kupitia mkakati huo  taasisi hiyo itafungua vituo vya kisomo katika mikoa 21 ya Tanzania Bara ili kutoa fursa kwa vijana na watu wazima wapate fursa ya kujifunza kusoma,kuandika na kuhesabu.

Kwa upande wa mgeni rasmi ambaye ndio amefungua mkutano huo Mbando amesema "Baraza la wafanyakazi ni takwa la kisheria na ambalo linawezesha taasisi kufanya kazi zake kwa ufanisi na kwa uwazi bila migogoro baina ya wafanyakazi na menejimenti na kwamba baraza hilo ni chombo kiachorahisisha utendaji kazi mahala pa kazi.

"Hivyo ni jukumu lenu wajumbe kuhakikisha kwamba maoni, ushauri na mipango ya baraza hili vinachangia katika kutela maendeleo ya taasisi ya elimu ya watu wazima na kuisaidia Serikali ya awamu ya tano kufikia malengo iliyojiwekea katika sekta ya elimu nchini.Vikao vya baraza la wafanyakazi vinasaidia kujenga uhusiano mzuri kati ya wafanyakazi na menejimenti na hatimaye kuleta mafanikio makubwa pale vinapotumika vizuri,"amesema.

Ameogeza binafsi anaifahamu taasisi hiyo kwa miaka mingi kutokana na elimu ya kuinua kisomo pamoja na elimu kwa umma kupitia madarasa ya kisomo na kampeni zake mbalimbali.Amefarijika kusikia taasisi  hiyo wameandaa mkakati wa kitaifa kuinua kisomo na elimu kwa umma nchini.

"Naamini mkakati huu utachangia katika kupunguza tatizo  la wasiojua kusoma na kuandika nchini kwani tatizo hilo limekuwa likongezeka mwaka hadi mwaka na ushauri wangu kwa Taasisi ni kuhakikisha fursa hiyo ya kisomo inaenda sambamba na fursa za kujifunza ujasiriamali na ufundi mbalimbali hasa katika viwanda vidogo vidogo,"amesisitiza.
 Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Dk.Kassimu Nihuka akizungumza kuhusu mafanikio na changamoto mbele ya wajumbe wa baraza hilo waliokutana leo jijini Dar es Salaam.
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mbando akizungumza leo wakati akifungua rasmi Mkutano wa Tisa wa Baraza la Wafanyakazi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Tisa wa Baraza la Wafanyakazi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima wakishiriki mkutano huo leo jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad