HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 6, 2018

Wafanyakazi Wanawake wa Vodacom Tanzania Foundation, Doris Mollel Foundation waadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutoa msaada hospitali ya Muhimbili

Wafanyakazi wanawake wa kampuni ya Vodacom Tanzania PLC na taasisi yake ya kuhudumia masuala ya jamii ya Vodacom Tanzania Foundation, leo wametembelea wodi ya wazazi katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutoa vifaa mbalimbali ,ukiwa ni mwendelezo wake wa kutoa vifaa vya kuokoa zaidi ya watoto 260 wanaozaliwa kabla ya wakati kila mwaka nchini.

Akiongea wakati wa kukabidhi vifaa hivyo na kutembelea wagonjwa, Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia alisema “Tunayo furaha kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu kwa kutembelea hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutoa msaada katika wodi ya wazazi vitakavyowezesha kupunguza vifo vya watoto wachanga. Tutaendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania za kuboresha sekta ya afya hususani kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga”.

Vifaa tiba mbalimbali vya kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) vilitolewa, baadhi ya vifaa hivyo ni vya kuwasadia watoto kupumua, kuongeza joto, kupima na kuratibu uzito kidijitali, pampasi na khanga, [oxygen concentrators, nebulizer machines, digital weigh scales, surfactants, infusion pumps and continuous positive airway machines, as well as Pampers and khangas].
 Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia (wa tatu kushoto) akikabidhi sehemu ya vifaa tiba maalum kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti), kwa Dkt. Mariam Kalomo aliyemwakilisha mgeni rasmi naibu waziri, wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, jinsia na watoto, Dr Faustine Ndugulile. Wa pili kulia ni Muasisi wa Taasisi ya Doris Mollel na Balozi wa Watoto Njiti, Doris Mollel.

Vodacom Tanzania Foundation inaelewa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wanawake nchini, wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua ndio maana imeamua kulivalia njuga changamoto zao na kuhakikisha vifo vya wanawake na watoto vinavyosababishwa na matatizo ya uzazi vinapungua.

“Kusaidia kuboresha afya za wanawake na watoto na lishe bora ni moja ya malengo ya taasisi yetu ya Vodacom Tanzania Foundation. Tunaamini msaada mkubwa unatakiwa kunusuru maisha ya wanawake na watoto kutokana na changamoto mbalimbali zinazowazunguka, tunaamini msaada huu utafanikisha kuleta matokeo chanya ya kuboresha na kuokoa maisha ya watoto wachanga,”alisema Mworia.
Msaada huu ni mwendelezo wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation, kutoa vifaa vya kisasa vinavyowezesha kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (Njiti) sambamba na miradi mingine inayolenga kuboresha afya ya uzazi na kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini, inayotekeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Baadhi ya miradi hiyo ni kuwasafirisha wanawake wenye ugonjwa wa Fistula hadi hospitali na kugharamia matibabu yao, kutoa jumbe za afya ya uzazi kwa wanawake wajawazito bure kupitia simu zao za mkononi za mtandao wa Vodacom sambamba na kuwawezesha wanawake wajawazito kuwahishwa katika vituo vya afya vyenye wataalamu wakati wanapokaribia kujifungua, kwa ajili ya kuokoa maisha yao na watoto wanaozaliwa.
 Akizungumza katika hafla hiyo, Dr Mariam Kalomo aliyemwakilisha mgeni rasmi naibu waziri, wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, jinsia na watoto, Dr Faustine Ndugulile aliwapongeza Vodacm Tanzania Foundation kwa msaada huo waliojitolea huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza pia.

“Nawashukuruni sana kwa msaada huu, maana tuna uhakika utapunguza vifo vya watoto wachanga kwa kiasi kikubwa, hiki mlichojitolea ni kikubwa mno kwa vile hospitali nyingi zinakabiliwa na upungufu wa vifaa tiba, kwa hiyo tunapopokea vifaa hivi tunakuwa na uhakika wa kuokoa maisha ya watoto wengi Zaidi,” alisema Dr Kalomo.

Kwa upande wake, Sister Zuhura Mahona aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili aliwahahakishia wafanyakazi wa Vodacom Tanzania Foundation kwamba vifa walivyojitolea vitatumika kwa usahihi kama vilivyoombwa.

Naye mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel , Doris Mollel aliwashukuru wafanyakazi wa Vodacom Tanzania Foundation kwa kujali watoto waliozaliwa kabla ya wakati na kuwaokoa kwa kuwaletea vifaa tiba hivyo.

 “Vifaa hivi ni muhimu sana kwa ajili ya watoto, kwa mfano ukimpatia mtoto hewa ya oxygen unakuwa umeokoa maisha yake ambayo labda angeyapoteza kwa kukosa hewa hiyo muhimu,” alisema Mollel.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka, ambapo hutumika kufikisha ujumbe wa kupambana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha kupata haki zao na usawa na kutoa wito wa kuhakikisha maisha ya wanawake yanaboreshwa katika Nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, lishe bora, afya ya uzazi, na maisha bora kwa ujumla.

Vodacom Tanzania Foundation inaendelea kusaidia Wanawake na Wasichana nchini pote kuboresha maisha yao katika Nyanja za afya, elimu bora na kuwawezesha kujikomboa kiuchumi kupitia ujasiriamali. Kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ya hapa nchini na wadau wengine, taasisi imesaidia zaidi ya miradi 120 mpaka sasa ikiwa imewekeza zaidi ya shilingi Bilioni 15 kwa ajili ya kuboresha maisha ya watanzania.No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad