Na Mwashungi Tahir, Maelezo Zanzibar.
WAZIRI Wa Nchi, Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa , Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alisema kabla ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar Kisiwa cha Tumbatu kulikuwa hakuna huduma yoyote ya maendeleo ikiwemo ya afya.
Akizungumza hayo Waziri huyo kwa niaba yaWaziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Issa Haji Gavu wakati wa ufunguzi ya wodi ya wazazi Tumbatu Gomani ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu.
Alisema huduma ya Afya kabla ya Mapinduzi ilikuwa adimu sana na kupatikana kwake ilikuwa lazima uifate Mkokotoni au kila alkhamis wanakuja madaktari kwa kutoa huduma ya afya kwa wananchi wa kisiwa hichi.
Hivyo Baada ya Mapinduzi Matukufu Marehemu Mzee Karume akatoa ahadi ya kujenga kituo cha afya kisiwani humo na huduma zikaanza kutolewa bila ya ubaguzi na wananchi wote wakaanza kufaidika na huduma hiyo.
Aliwaomba kuitumia fursa hii akina mama kwa kujifunguliya katika kituo hicho ambacho kina vifaa vyote vya huduma ya uzazi , na kuacha kujifunguliya majumbani kwani kunaweza kuhatarish afya ya mama na mtoto.
Aidha alisema hii ni ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh Ali Mohammed Shein katika kutimiza ahadi zake za kuwapelekea wananchi wake huduma zilizo muhimu ikiwemo ya Afya katika maeneo ya mjini na vijijini ikiwa ni sera na ilani ya Chama cha Mapinduzi .
“Tuyatunze, tuyaenzi na tuyadumishe Mapinduzi yetu matukufu 1964 kwani ndio yaliyotukomboa katika madhila mbali mbali hadi kufikia hapa tulipo”.Alisema Waziri huyo.
Pia Waziri huyo aliahidi kuongeza vitanda 10 vya kujifunguliya pamoja na magodoro ili lengo kuiboresha Zaidi huduma hiyo.
Nae Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alisema haya yote ni Matunda ya Mapinduzi Matukufu na jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya awamu ya saba ya Rais wa Zanzibar Dr Ali Mohammed Shein kwa kuwajali wananchi wake kwa kuwasogezea huduma mbali mbali za maendeleo ikiwemo hii ya afya bora.
Waziri Kombo na Wizara yake, amewaahidi kuwapelekea huduma zote kila panapostahiki ikiwemo dawa kwa wakati , na pia kuwanasihi wafanyakazi wa kituo hicho kuwa na maneno mazuri katika kuwahudumia wagonjwa pale wanapofika katika kituo hicho.
“Maneno mazuri peke yake ni lugha ya faraja kwa mgonjwa, tayari unamjenga matumaini na inampa amani na kuwa ni nusu ya tiba kwa upande wake mgonjwa huyo”. Alisema Waziri huyo.
Wakisoma risala yao wananchi wa kisiwa cha Tumbatu Gomani wamesema wanamshukuru Mh. Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohammed Shein kwa kuwapelekea mandeleo katika kisiwa hicho ikiwemo huduma za afya bora na wanaahidi watakitunza na kukienzi na kuthamini juhudi zake za kuwajali wananchi wake.
Wakitoa changamoto wameiomba wizara ya Afya kuwapatia madaktari kwa vituo vyote viwili vilivyopo Tumbatu Gomani na Jongowe, kupatiwa boti ya kisasa ya kusafirisha wagonjwa na wafanyakazi iwapo ikitokea dharurua, na kuwekewe vifaa vya kisasa vinavyoendana na uzuri wa jengo lenyewe. Jumla ya shilingi 221, 119 zimetumika kwa gharama za ujenzi pamoja na vifaa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe.Haji Omar Kheir kwa niaba ya Waziri wa Nchi ya Ofisi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Issa Haji Gavu akifungua pazia akiashiria kufungua Wodi ya Wazazi Kituo cha Afya Tumbatu Gomani (Picha na Kijakazi Abdalla Maelezo )
No comments:
Post a Comment