Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mheshimiwa Regina
Chonjo amewataka vijana kuonyesha vipaji vyao vya soka na kutambua kuwa mchezo huo
ni fursa nzuri inayoweza kuwapa maisha bora na kusaidia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Chonjo aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mashindano ya soka ya vijana
chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars kwa mkoa wa Morogoro uliofanyika kwenye
uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa mchezo huo.
“Napenda kutumia fursa hii kutoa rai kwa wazazi na walezi kuwahamasisha vijana kushiriki
michuano hii ili kuendeleza vipaji vyao na kusaidia juhudi za serikali za kuinua kiwango cha
mchezo wa soka hapa nchini”, alisema.
Zaidi ya wachezaji 120 walihudhuria uzinduzi huo
Alisema mbali ya kuwa burudani, mpira wa miguu pia hudumisha amani, umoja, urafiki,
udugu miongoni mwa viongozi na wachezaji na kuwafanya vijana kuwa wakakamavu,
wachangamfu na wenye afya bora. “Lakini muhimu zaidi mpira wa miguu ni chanzo cha ajira
kwa vijana wengi duniani”, alisema .
Aliwataka viongozi wa soka mkoa wa Morogoro kufuatilia kwa karibu michuano hiyo na
kuchagua wachezaji wenye vipaji ili kuuwezesha mkoa huo kufanya vizuri katika fainali za
Taifa za Airtel Rising Stars zinazotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba
6 hadi 11.
Alisema michuano ya Airtel Rising Stars imekuwa ni jukwaa la kusaidia kubaini wachezaji
wenye vipaji kutoka sehemu mbalimbali ambao bila mashindano haya wangeweza kupotea
hivi hivi. Aliwataka viongozi wa soka mkoa humo kushirikiana na shirikisho la soka nchini
(TFF) kuwalea na kuwaendeleza vijana wanaopatikana kupitia Airtel Rising Stars.
Akiongea katika hafla hiyo ya ufunguzi, mwenyekiti wa wa chama cha Soka mkoani
Morogoro Pascal Kihanga ambaye pia ni Mustahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro
aliwataka vijana kucheza kwa kujituma ili kuweza kuchaguliwa kuunda timu ya mkoa.
Kwa upande wake, Meneja wa Airtel mkoa wa Morogoro Omar Bongo alisema kuwa
kampuni ya Airtel inajivunia kuweza kupata fursa ya kutoa mchango katika soka la Tanzania.
“Airtel Rising Stars imekuwa chimbuko la wachezaji wa timu za Taifa na klabu hapa nchini”.
Tunaona fahari kuweza kupata fursa ya kudhamini soka nchini Tanzania“alisema Bongo.
Hafla hiyo ya ufunguzi ilishuhudia mchezo wa ufunguzi kati ya Moro Kids na Techforty
ambapo Moro Kids waliibuka na ushindi wa 2-0. Katika mchezo mwingine, Mwere Kids
iliishinda Kizuka 2-1.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mheshimiwa Regina Chonjo akikagua timu wakati wa
ufunguzi wa Airtel Rising Stars mkoa wa Morogoro kwenye uwanja wa Jamhuri jana.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mheshimiwa Regina Chonjo akipiga mpira kuashiria ufunguzi
Airtel Rising Stars mkoa wa Morogoro kwenye uwanja wa Jamhuri jana.
No comments:
Post a Comment