Waziri Elimu Wazira wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi Mhe. Mhandisi Stella Manyanya akijibu maswali kutoka kwa wabunge mbalimbali katika kipindi cha maswali na majibu katika kikao cha Tano cha Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma Picha na raymond Mushumbusi MAELEZO
Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi inatarajia kujenga Vyuo vya Ufundi (VETA) kwa kila wilaya ili kutoa fursa kwa wananchi wengi hususani vijana kupata mafunzo mbalimbali ya ufundi yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi na kujenga taifa.
Akijibu swali la Mbunge wa Lupa Mhe.Victor Kilasike Mwambalaswa (CCM) kuhusu ujenzi wa vyuo vya VETA kwa kila Wilaya ambapo Wilaya ya Chunya ni moja kati ya Wilaya kumi za mwanzo zilizo katika mpango wa ujenzi wa vyuo hivyo wakati wa maswali na majibu, Wizara ya Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi Mhe. Mhandisi Stella Manyanya amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwa na Chuo Cha VETA sio kwa wilaya ya Chunya tu bali kwa Wilaya zote nchini, tayari maandalizi ya awali ya ujenzi wa chuo cha VETA ikiwa ni pamoja na kufanya utambuzi wa stadi zinazohitajika katika vyuo hivyo.
“ Natoa wito kwa wabunge katika majimbo yao kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya zote watafute ardhi kwa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivi ili hata mipango ya ujenzi ikikamilka ikute eneo lipo tayari kwa kuanza utekelezaji wake”Alisema Mhe.Manyanya.
Mhe. Mhandisi Stella Manyanya amesema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeshateua wataalamu elekezi watakaoshindanishwa kutayarisha andiko la jinsi ya kuifanya kazi ya kubuni majengo na kupata gharama ya kazi hiyo ili kuanza ujenzi mara moja.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imejipanga kutoa elimu bora ya ufundi yenye kuleta ufanisi katika maendeleo ya ufundi stadi nchini ili kuwawezesha wahitimu kupata ujuzi ulio bora kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment