Mkurugenzi Mkuu wa Helvetic Solar Contractors Eng. Patrick Ngowi akiwa na mwenyeji
wake Mkurugenzi Mkuu wa ITV na Radio One Bi. Joyce Mhavile alipofika katika
ofisi hizo mapema leo kwa ajili ya mazungumzo na kuhojiwa katika kipindi
cha Business Edition, kitakachorushwa Ijumaa hii saa 2 na dakika 15
usiku, Capital TV.
Mkurugenzi Mkuu wa Helvetic Solar Contractors Eng. Patrick Ngowi
ameendelea kutoa rai kwa vijana nchini Tanzania kuwa na moyo na bidii
ili kuweza kutimiza ndoto zao za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.
Eng. Ngowi ambaye pia ni mshindi wa ‘Forbes 2013: 30 under 30: Africa’s
Best Young Entrepreneurs’ alisema maneno hayo mapema leo katika mazungumzo
na Mkurugenzi Mkuu wa ITV na Radio One Bi. Joyce Mhavile alipofika kufanya
ziara na mahojiano maalum katika kituo hicho.
“Vijana wa kitanzania wanafursa nyingi sana katika nchi yetu, imefika
wakati sasa vijana wajitambue kwamba wanaweza kutimiza ndoto zao kadiri
bidii zao zitakavyowatuma. Kwa mfano, mi nilianza na mtaji wa shilingi
milioni mbili, lakini hivi sasa nilipofikia biashara yangu imekua na
nimeweza kufanya maajabu makubwa katika soko ukizungumzia swala ya nishati
ya jua,” alisema Eng. Ngowi.
Aliongeza, “Kinachotakiwa ni kuwa mbunifu katika biashara unayofanya,
kuwa na ujasiri pamoja na umakini wa kile unachokipenda na pale unapotaka
kufika. Yote yanawezekana na kijana yeyote anaweza fanikiwa.”
Pamoja na hayo Eng. Ngowi aliwapongeza sana IPP media kwa mafanikio
yao waliyopata katika kipindi chote tangu kianzishwe, ikiwemo tuzo ya
‘Number 1 Super Brand’ katika Afrika Mashariki hivi karibuni.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa ITV na Radio One Bi. Joyce Mhavile alimpongeza
kwa mafanikio yake na kumshukuru sana Eng. Ngowi kwa ugeni wake.
Kampuni ya Helvetic Solar
Contractors ambayo Eng. Ngowi ni muasisi wake, mwaka jana iliweza kushinda nafasi ya kwanza katika
mashindano ya ‘100 Top Mid-Sized Company in Tanzania.’ Mwezi Machi
mwaka huu Eng. Ngowi aliweza kuorodheshwa katika kundi la wajasiriamali
bora 30 vijana barani Afrika wenye umri chini ya miaka 30 ijulikanayo
kama ‘Forbes 30 under 30: Africa’s Best Young Entrepreneurs’.
Picha na habari na Amani Nkurlu.
No comments:
Post a Comment