Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala,Mh. Jerry Slaa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mchakato wa uanzishwaji wa huduma za matibabu kwa wananchi kupitia mpango mpya wa Tiba kwa Kadi (TIKA) kwa madiwani wa Manispaa hiyo yanayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao ni msimamizi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) inayoendelea hivi sasa kwenye ukumbi wa Arnautoglo,Ilala jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Khamis Mdee akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya mchakato wa uanzishwaji wa huduma za matibabu kwa wananchi kupitia mpango mpya wa Tiba kwa Kadi (TIKA) kwa madiwani wa Manispaa ya Ilala,Jijini Dar es Salaam leo.
Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Khamis Mdee akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo ya mchakato wa uanzishwaji wa huduma za matibabu kwa wananchi kupitia mpango mpya wa Tiba kwa Kadi (TIKA) kwa madiwani wa Manispaa ya Ilala,Jijini Dar es Salaam leo.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala,Ellioth Mwasambite akiwatambulisha baadhi ya Madiwani wa Manispaa ya Ilala waliofika kwenye Mafunzo hayo leo.
Wakurugenzi na Maofisa wa NHIF wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mgeni Rasmi.
MC wa shughuli hiyo akiongoza shughuli hiyo.
Mh. Meya akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Khamis Mdee wakati alipokuwa akiwasili ukumbini hapo.
Baadhi ya Madiwani wa Ilala waliofika kwenye Mafunzo hayo leo.
Picha ya Pamoja.
Na Mwandishi Wetu
MANISPAA ya Ilala imedhamiria kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi wake kupitia mpango mpya wa Tiba kwa Kadi (TIKA) unaotarajiwa kuanzishwa hivi karibuni baada ya kupitishwa kwa sheria ndogo na Hati Rasmi.
Hatua hiyo imejulikana wakati wa mafunzo ya mchakato wa uanzishwaji wa TIKA kwa madiwani wa Manispaa hiyo yaliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao ni msimamizi wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Akifungua mafunzo hayo, Mstahiki Meya Jerry Slaa alisema kuanzishwa kwa mpango huo kutasaidia sana kuondokana na dhana ya kulipia huduma kila wanapokwenda kwenye vituo vya kutolea matibabu kwa sababu watapata fursa ya kuchangia mara moja kwa mwaka.
“Suala la matibabu kwa bahati mbaya limetekwa na linataka kufanywa lionekane la kibiashara zaidi. Tusipokuwa makini gharama za matibabu zitakuwa zinapanda kila kukicha kwa visingizio mbalimbali na hilo litawapa wakati mgumu zaidi wnanchi wetu kumudu gharama hizo,”
“Inapotokea wanajitokeza wadau kama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kusaidia suala hili hatuna budi kuwaunga mkono na kushirikiana nao katika hatua hii muhimu ili utaratibu huu uanze mara moja,” anasema Slaa.
Akizungumzia manufaa ya TIKA, alisema ni pamoja na kuwashirikisha wananchi wenyewe katika usimamizi wa huduma za matibabu lakini pia utapunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko ya rushwa katika vituo vya matibabu hasa yale ya malipo ya papo kwa papo.
“Hata kwa wale watendaji wanaounga mkono sana utaratibu wa malipo ya papo kwa papo tunatakiwa kuwaangalia kwa jicho jingine kwani utaratibu huo umepitwa na wakati na unaotakiwa kwa sasa ni matumizi ya kadi wakati wa kupata matibabu na ukweli ni kwamba malipo ya papo kwa papo hayamsaidii mwananchi wetu tunayemwakilisha,” alisema Slaa.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wadau wote kuhakikisha wanauelewa mpango huo na hasa katika eneo la usimamizi wa mapato na matumizi katika mpango huo ili fedha hizo ziweze kutatua changamoto za huduma za matibabu kama ukosefu wa dawa.
“Ilala tujielekeze katika uanzishaji wa TIKA na tuione hatua hii kama jawabu la kutatua changamoto sugu ya huduma ya dawa katika vituo vyetu, hii inawezekana kwa kuwa ipo mifano hai ya wenzetu waliofanikiwa kuondoa tatizo sugu la dawa,” alisisitiza Slaa.
Kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulioongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Hamis Mdee, alisema kuwa umuhimu mkubwa wa TIKA ni kusaidia kutatua changamoto ya upatikanaji rasilimali fedha katika utoaji wa huduma kwa wananchi na uhakika wa matibabu kwa wakazi wa Manispaa.
“Wananchi watapunguza mzigo wa kutafuta fedha za matibabu pindi wanapougua kwa kuwa mpago huu unamtaka mwananchi kuchangia kabla ya kuugua lakini pia mwananchi anapata ushiriki katika kupanga juu ya huduma za afya kupitia bodi na Kamati,” alisema Mdee.
Aidha Mdee alitumia mwanya huo kuwaomba wadau wa mfuko huo kufanya maandalizi ya kutosha ya upatikanaji wa kadi za wanachama, kutambua vituo vya kutolea huduma na usimamizi wake na Manispaa iweke mkakati wa kuelimisha wananchi.
Baada ya kufanyika kwa mafunzo hayo ya utangulizi ya mchakato wa kuandaa Sheria ndogo pamoja na Hati Rasmi ya TIKA kwa Manispaa ya Ilala utaanza.













No comments:
Post a Comment