HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 9, 2012

Halmashauri wekeni sheria ya CHF-RC

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Hamis Mdee akifafanua jambo wakati wa kutoa msaada wa mashuka 150 katika Hopsitali ya Halmashauri ya Mji wa Babati kama mchango wake ndani ya jamii, kulia ni Mjumbe wa Bodi ya NHIF, Mwanaidi Mtanda.
Wagonjwa wakiwa wamefunikwa mashuka yaliyotolewa na NHIF katika Hospitali ya Maunt Meru,Arusha muda mfupi baada ya kutolewa kwa msaada huo.
Viongozi wa NHIF wakipata maelezo kwa Mganga wa Kituo cha Afya cha Oltrumet walipotembelea na kugawa mashuka.
Mjumbe wa Bodi ya NHIF,Mwanaidi Mtanda akikabidhi koti kwa mwendesha pikipiki mkoani Arusha ikiwa ni mchango wake ndani ya jamii hasa kwa kutambua makundi.
.Mkuu wa Mkoa wa Manyara Erasto Mbwiro akifungua mkutano wa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima
ya Afya mkoani Manyara leo.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,Mwanaidi Mtanda akitoa salaam za Bodi kwa wadau wa Mfuko katika Mkutano uliofanyika Mkoani Manyara leo.
Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji, Deusdedit Rutazaa akitoa mada kwa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya mkoani Manyara leo.
Wadau wa NHIF mkoani Manyara wakifuatilia mada katika mkutano wa siku ya wadau.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,Hamisi Mdee na Mjumbe wa Bodi Mwanaidi Mtanda wakiwa na wadau wakifuatilia mada.
Kikundi cha waendesha piki piki mkoani Arusha wakiwa wamevalia makoti ya usalama barabarani yaliyokabidhiwa na NHIF baada ya kujiunga na CHF.

Na Mwandishi Wetu, Manyara

HALMASHAURI mkoani Manyara zimetakiwa kuangalia uwezekano wa kuweka sheria ndogo zinazoelekeza ulazima wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote.

Agizo hilo lilitolewa jana mkoani hapa na Mkuu wa Mkoa huo, Erasto Mbwiro wakati akifungua Mkutano wa wadau ambao umekutanisha wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, watoa huduma, wabunge, madiwani na wadau wengine.

Alisema kuwa Mfuko huo wa Afya ya Jamii hauwezi kuwa na mafanikio ya kutosha endapo hapatakuwa na sheria inayomlazimisha mwananchi kujiunga nao hivyo akawataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuliangalia hilo kwa makini ili liweze kufanikiwa.

"Hakuna mtu anayependa kuumwa na ugonjwa unakuja wakati ambao hata hela hauna hivyo ni lazima huu Mfuko tuuchangamkie ili wananchi wetu wapate uhakika wa matibabu ...bila afya njema hakuna maendeleo na maadui umasikini na ujinga ndiyo yatapata nafasi," alisema Mbwiro.

Pia alizitaka Kamati za Afya na Elimu kuhakikisha zinafanya kazi ya kuwaelimisha wananchi kuhusiana na Mfuko huu ili wajue faida zake na wahamasike kujiunga nao.

"Haiwezekani Manyara tukawa kwenye asilimia tatu ya kaya zote zilizoko mkoani hapa na wakati kila kaya ina mifugo ya Ng'ombe na kuku...na mchango wa Mfuko huu ni kati ya elfu kumi au shirini ambazo zinaweza kutokana na kuuza hata kuku mmoja tu,' alisema Mkuu huyo.

Pamoja na hayo, hakusita kuzitaka Halmashauri kuweka mikakati ya uboreshaji wa huduma za matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya ili wananchi wasikate tamaa ya kuchangia.

Alisema kuwa endapo dawa zitapatikana katika vituo hivyo, idadi kubwa ya kaya zitahamasika kujiunga na hatimaye Watanzania wengi kuingia kwenye utaratibu wa Bima ya Afya.

"Tumieni fursa ya Mikopo ya Vifaa tiba na ukarabati wa majengo inayotolewa na NHIF, hii itasaidia sana kuboresha huduma zetu na wananchi watavutika kutibiwa," alisisitiza.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bi. Mwanaidi Mtanda alisisitiza suala la kutumia fursa ya mikopo ya vifaa tiba kwa kuwa Mkoa wa Manyara ni kati ya mikoa ambayo haijatumia fursa hiyo.

"Hospitali ya Mkoa na za Wilaya ziangalie uwezekano wa kuwa na maduka ya dawa ili wanachama na wananchi wasiondoke hospitali bila ya kuwa na dawa lakini pia mapato yatokanayo na dawa yatabaki kwenu na mtaendelea kuboresha zaidi," alisema.

Mtanda pia alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa kiserikali, kisiasa na madhehebu ya dini kusaidia katika suala la uhamasishaji kwa wananchi kujiunga katika utaratibu wa Bima ya Afya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad