HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 29, 2012

Taifa Stars yatoka sare ya bao 1-1 na msumbiji leo

Mshambuliaji wa Taifa Stars, Mrisho Ngasa (kushoto) akichuana na beki wa Msumbiji, Almiro Lobo katika mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika uliochezwa jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars),Shadrack Nsajigwa akiwatoka mabeki wa timu ya Taifa ya Msumbiji (Mambas) katika mchezo uliopigwa leo kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wa kuwania tiketi ya kufuzu kucheza Mataifa ya Afrika 2013 nchini yatakayofanyika nchini Afrika Kusini.Timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1.
Golikipa wa timu ya taifa ya Msumbiji, Joao Raphael akiwa chini huku mshambuliaji wa Stars, John Boko akikosa bao la wazi baada ya kubaki yeye na kipa tu langoni.
Mshambuliaji wa Timu ya Taifa Stars, Vincet Barnabas akimtoka Beki wa Timu ya Taifa ya Msumbiji,Stelio Ernesto.
Mwinyi Kazimoto akishangilia bao aliloifungia Stars na kuyafanya matokeo ya mechi hiyo kuwa 1-1
Kocha wa Stars Jan Poulsen (kulia) akipeana mkono na Kocha wa Msumbiji, Gert Angels mara baada ya mpira kumalizika.

Na Francis Dande

Timu ya soka ya Tanzania Taifa Stars, leo imeshimdwa kutamba mbele ya timu ya Taifa ya Msumbiji 'Mamba's kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kutoka sare ya 1-1 katika pambano la kuwania kufuzu Mataifa Afrika 2013 nchini Afrika Kusini.

Wiki moja iliyopita, Taifa Stars iliambulia sare ya 0-0 dhidi ya DRC katika mechi ya kujipima nguvu, huku gonjwa sugu la kufumania nyavu likionekana kushindwa kutafutiwa ufumbuzi na Poulsen kiasi cha kukigharimu kikosi hicho leo. 

Pambano hilo lililopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lilikuwa ni la kwanza kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Mataifa Afrika 2013 nchini Afrika Kusini, ambapo Stars imetoka sare ya bao 1-1 na Msumbiji. 

Stars iliyoingia dimbani ikitoka kuchagizwa na wakali kadhaa walioiwezesha Tanzania kufuzu fainali za mwaka 1980, ilionekana dhahiri kutokuwa katika mfumo wa kuweza kuibuka wababe, ikimtumia mshambuliaji mmoja John Boco ambaye alikosa mabao ya wazi.

Pambano lilianza kwa muendelezo wa kosakosa miongoni mwa safu ya mbele ya Stars, ambako dakika ya 15, John Boko alikosa bao, kabla ya kipa wa Stars Juma Kaseja kuokoa shuti la Clesio Bauque aliyekuwa mwiba katika safu ya ulinzi. Bao la Msumbiji lilifungwa na Clesio Bauque dakika ya 22, baada ya kuwatoka mabeki wa Stars kumpoteza Juma Kaseja langoni, kabla ya Mwinyi Kazimoto kusawazisha dakika ya 40. 

Kazimoto alifunga bao hilo kwa shuti la nje ya boksi, akimalizia pasi safi ya Vicent Barnabas. Hadi mwamuzi Moahammed Farouk Misri anapuliza filimbi ya mapumziko, timu zilikuwa sare kwa bao 1-1. 

Kipindi cha pili licha ya Stars kufanya mabadiliko kwa kuwatoa Nozar Khalfan, Abdi Kasim na Vicent Barnabas na kuwaingiza Mrisho Ngasa, Salum Aboubakar na Husein Javu, bado iliendelea kukosa mabao kiashi cha Boco kuzomewa na pambano kumalizika kwa sare hiyo inayoweka shakani nafasi ya Tanzania kusonga mbele.

Taifa Stars: Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Stepheno Mwasyika, Juma Nyoso, Aggrey Morris, Shabani Nditi, Nizar Khalfan, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Abdi Kassim ‘Babi’ na Vincent Barnabas.

Msumbiji: Joao Raphael, Edson Sitoe, Zainadine Junior, Eduardo Jumisse, Jerenias Sitoe, Elias Pelembe, Clesio Bauque, Francisco Muchanga, Stelio Ernesto, Francisco Massinga na Almiro Mohammed.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad