HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 5, 2011

Neno La Leo: Ukimwona Mtu Tajiri, Tamani Kuwa Kama Yeye, Lakini....

Ndugu zangu,

Kwenye Uchina ya Kale kulikuwa na mwanafalsafa kwa jina la Comfucius. Katika mafundisho yake mengi aliyopata kumpa mwanafunzi wake Tzu Kung mojawapo linahusu dhana ya utajiri na mahusiano yake na umasikini.

Comfucius anasema; ukimwona mtu tajiri (aliyefanikiwa kimaisha),basi tamani kuwa kama yeye, lakini, ukimwona aliye maskini, basi, jitafakari wewe mwenyewe.

Kwa mwanafalsafa Comfusius, dhana ya utajiri haikuwa na maana kuwa na mali pekee, bali, pamoja nazo, ni uwezo wa mtu kuishi maisha adilifu na yenye fadhila (virtues). Na katika fadhila zote, ile ya unyenyekevu na ukweli ndio chanzo cha fadhila nyingine zote.

Umaskini vilevile, yumkini unaweza kuwa na maana ya kukosa mali na uadilifu. Ndio, mwanadamu waweza kuwa na mali lakini ukakosa uadilifu. Ni dhahiri, katika hali hiyo, hata mwenye mali naye ni maskini sana.

Ndugu zangu,

Nayaandika haya baada na huku nikiendelea kusoma alama za ukutani.
Kuna kitu kinatokea katika jamii yetu. Wengine wanakiona, wengine hawakioni. Na kuna wanaoonyeshwa , lakini wanashindwa kukiona. Tunafanyaje?

Ndugu zangu,
Hakuna kitu kingine bali ni watu ndio wenye kuifanya nchi. Kuna kitu kimetutokea waTanzania. Kinaendelea kuota mizizi. Na kwa vile kitu ndicho hufanya vitu, basi, mimi naviona vitu vya hovyo hovyo vikitokea katika jamii yetu. Na pengine, kwa vile tumeanza kuwa na hulka za hovyo hovyo, basi, vinavyotokea hatuvioni kuwa ni vya hovyo hovyo.

Naam, vinatokea kila leo, na kuna wenye kusimama kuvitetea vitu hivyo vya hovyo hovyo. Ni kuanzia namna tunavyouza rasilimali zetu na wenye kuuza, ni viongozi wetu waliogeuka ’ madali’ wa kutanguliza tenipasenti. Hawa wa kundi la pili ndio matajiri wetu wapya waliopungukiwa chembe nyingi za uadilifu, hivyo basi, nao ni masikini.

Na tumeimbiwa sana, kuwa nchi yetu ni maskini (japo wanamaanisha kipato pekee) na wanasahau au hawaju kuwa sisi ni maskini zaidi kwenye maadili.

Ndugu zangu,

Na tunavyoelekea sasa kwenye miaka hamsini ya Uhuru , tujifunze kutoka kwa mwanafalsafa Comfusius . Kwamba katika umasikini wetu huu kama taifa, basi, walau tujitahidi kujitafakari tulivyo huku tukiwaangalia wenzetu waliopiga na wanaondelea kupiga hatua za mafanikio ya kiuchumi.

Ndugu zangu,
Oneni kule Marekani. Hawa ni matajiri wa kipato. Wanafanya kazi usiku na mchana kutimiza ndoto ya taifa lao. WaMarekani wanaijua ndoto yao na huungana dhidi ya yeyote anayetaka kuikwamisha. Ni pengine ni katika kutimiza ndoto hiyo sisi tunalalamika kuwa Marekani ni taifa baya.

Tujiulize; ni taifa gani litaishi bila kuwa na ndoto na haja ya kuwa na maslahi ya kudumu? Hivi, ni nini ndoto na maslahi ya kudumu ya Tanzania? Je, ni WaTanzania wangapi wakiwemo viongozi wanaijua sera ya Tanzania inapohusu uhusiano wake na mataifa mengine?

Fikiri, tumepeleka majeshi yetu kuzikomboa nchi nyingine, lakini, ni vigumu kuona tumepata nini kiuchumi ukiacha sifa ya kuwa ni taifa karimu.

Angalia Rwanda. Ni kanchi kadogo sana lakini kameshajua ni nini maana ya kuwa na ndoto na haja ya kuwa na maslahi ya kudumu . Ndio maana hukusikia Rwanda ikitafuna maneno katika kuitambua Serikali ya Mpito ya Libya.

Leo Rwanda wako ndani ya DRC na wana maslahi ya migodi ya madini ya huko. WanyaRwanda wale wamepenya hadi Uganda na Burundi. Na nani atabaisha, kuwa WanyaRwanda wamepenya hata kwenye uchumi wetu.

Ndugu zangu,
Tumekuwa ni watu wa hovyo hovyo. Tupo kama hatupo. Tunayakimbia mambo ya kimsingi kwa taifa letu. Tumejikita zaidi kwenye hoja nyepesi nyepesi ikiwamo fitina na majungu. Ndio, WaTanzania tunabaguana kisiasa na kuna ambao, piga ua, watahakikisha tunapata Katiba Mpya ya hovyo hovyo ili tuendelee na mambo yetu ya hovyo hovyo.

Hatujachelewa, na tujifunze kutamani kuwa kama walio matajiri(katika maana ya mwanafalsafa Comfucius).

Ndugu zangu,

Naomba kuwasilisha hoja.

Maggid Mjengwa
Iringa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad