ZANZIBAR
JUMATANO, SEPTEMBA 7, 2011. Zaidi ya watoto 400 wenye umri kati ya
miaka mitano na 17, walipotea mjini Zanzibar katika kipindi cha siku nne
za maadhmisho ya Siku Kuu ya Iddi El Fitri ya kumalizika kwa mfungo wa
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Taarifa
ya Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina,
imesema kuwa karibu watoto wote waliokuwa wamepotezana na ndugu na jamaa
zao wakati wa sherehe hizo, walifikishwa katika vituo mbalimbali vya
Polisi mjini Zanzibar na kufanyiwa utaratibu wa kurejeshwa makwao.
Akizungumzia
matukio yaliyojitokeza katika kipindi hicho, Kamanda wa Polisi wa mkoa
wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amesema kuwa
ongezeko la upotevu wa watoto hao ilikuwa kubwa mno ikilinganishwa na
siku kuu nyingine kama hizo katika miaka iliyopita.
Kamanda
Azi amesema kuwa Polisi walilazimika kumhoji kila mtoto ili kujua
anakoishi na pale ilipowawia vigumu watoto hao kujitambua pia walihojiwa
ili kutaja shule ama madrasa wanazosoma jambo ambalo lilirahisisha kila
mtoto kurejeshwa makwao.
Amesema
watoto wengi hawakufahamu maeneo waliotoka kwa majina lakini walizitaja
shule na madrasa wanazosoma jambo ambalo alisema lilirahisisha katika
kuwafikisha watoto hao makwao kwa urahisi.
Amesema
wakati wa siku kuu hiyo Polisi pia walifanikiwa kukamata kiasi kikubwa
cha mihadarati na pombe ya moshi maarufa kama Pombe ya Tende na kuharibu
mapipa 12 yaliyokuwa yakitumika kupikia pombe hiyo.
Kamanda
Aziz amesema pia kuwa Polisi waliyakamata magari 148 yakiwemo ya abiria
na mizigo kutokana na makosa mbalimbali yakiwemo ya kutozingatia
matumizi salama ya barabara na madereva wake na wamiliki wa vyombo hivyo
wameanza kufikishwa mahakamani.
Siku
Kuu ya Iddi El-Fitri, ndiyo Siku Kuu kubwa kuliko zote katika Visiwa
vya Unguja na Pemba na husherehekewa kwa muda wa siku nne au zaidi
ikilinganishwa na siku kuu nyingine visiwani humo ambapo watoto na watu
wazima huonekana mitaani na katika maeneo mbalimbali ya burudani katika
viwanja vya wazi wakiwa na mavazi mapya na ya heshma.
No comments:
Post a Comment