HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, September 24, 2011

Rais Kikwete awataka Watanzania waishio Marekani wasibweteke na badala yake watumie fursa zinazotolewa na serikali ili kupeleka maendeleo nyumbani


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia katika mkutano huo.

Na Mindi Kasiga,Virginia-Marekani.

Watanzania waishio Marekani wameaswa wasibweteke na badala yake watumie fursa zinazotolewa na serikali ili kupeleka maendeleo nyumbani. Hayo yamesemwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tatu wa Baraza la Watanzania Waishio Marekani leo mjini Dulles, Virginia na Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwenye hutuba yake ya ufunguzi, Rais Kikwete aliwaambia Watanzania kuwa kila mmoja anawajibu wa kusaidia kusukuma gurudumu la maendelo nchini Tanzania kwani ni wajibu wa kila Mtanzania na si Serikali peke yake.

Aidha Rais Kikwete aliwaasa Watanzania wawe ni mfano wa kuigwa na mataifa mengine wakiwa ugenini. Wawe Raia wazuri nchini Marekani, watii wa sheria, wasaidie kusomesha ndugu zao nyumbani ili mafanikio waliyoyapata kwa kuishi ughaibuni, yafike hadi kijijini walipotokea kwa kuwasaidia wale waliowaacha.

Pia Rais Kikwetealiwasisitiza Watanzania walio nje kuwa kamwe wasisahau walipotoka, nyumbani, ikiwezekana waanze kutafuta ardhi na kujenga nyumba za kuishi Tanzania.

“Badala ya kulalamika tu na kuandika kwenye blogs, ni wakati sasa muanze kusaidia kuwekeza nyumbani, kwani nchi ni yetu sote, hakuna mliyemkabidhi alete maendeleo ili yakishapatikana ndio mrudi nyumbani” alifafanua Rais Kikwete huku akishangiliwa na umati wa watanzania uliofurika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Marriot.

Naye Waziri mwenye dhamana ya kuratibu masuala ya Watanzania waishio ughaibuni, Mheshimiwa Bernard Membe, alisema Rais Kikwete ana nia ya dhati, kusaidiana na Watanzania nje ya nchi ili kuhakikisha maendeleo yao yanawanufaisha wao pamoja na Tanzania.

Akisisitiza jitihada za serikali na za Rais Kikwete katika kuhalalisha suala la uraia pacha, ambalo ni mojawapo ya kilio kikubwa cha Watanzania waishio ughaibuni, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alisema ingawa ni suala la kikatiba, lakini Serikali inategemea kuwa ndani ya kipindi hiki ambapo katiba inapitiwa na kufanyiwa mabadiliko, ndio wakati muafaka wa suala hili kujadiliwa kwa kina ili likamilishwe na kuingia kwenye katiba mpya.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na mabalozi wa Tanzania nchini Marekani Balozi Mwanaidi Maajar na Balozi Ombeni Sefue ambao nao walizungumzia sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara wakisema Watanzania wana kila sababu ya kuringa kwani mafanikio ya miaka 50 ni ya kujivunia.

Mkutano huo wa siku tatu uliodhaminiwa na makampuni ya kitanzania tu, umevutia Watanzania zaidi ya 500 kutoka pande mbalimbali za Marekani, na unatarajiwa kujadili njia za kukabiliana na changamoto za wana diaspora ili kuchangia maendeleo na kukuza pato la nchi.

3 comments:

  1. Mtembelee JK kwenye FESIBOOK yake mapicture kibao na wakina 50cent na wengineo.

    ReplyDelete
  2. Mr President kama untaka ku encourage watu ku invest nyumbani ungeanza na bandarini,watu wanavunjwa moyo na mamlaka ya bandari kwani zengwe linaloendelea hapo unapoleta mzigo wako unavunjika moyo and you loose faith with the idea za kuendelea kuleta mzigo mwengine. We need more actions and few words from the govt!!

    ReplyDelete
  3. Hii serikali yetu ni sawa na kutia sukari baharini,tuta comment lakini atuta badirisha kitu.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad