Mshindi wa kwanza mbio za walemavu wa ngozi (albino),
Maneno Enock akivalishwa medali na mwakilishi kutoka Airtel Jane Matinde
MWANARIADHA
Godfrey Chacha wa Mara jana aliibuka mshindi wa mbio za Rock
City Nusu Marathon 2011 upande wa wanaume akiwapiku wenzake zaidi ya
100 kwenye mbio hizo zilizofanyika jijini Mwanza.
Chacha
alitumia muda wa 61.03.44 na kutwa nafasi hiyo, wakati upande wa
wanawake Jackline Juma kutoka Arusha alitwaa ushindi wa kwanza akitumia
muda wa 1:15.22 baada ya kuwashinda wenzake 30.
Kwa
upande wa mbio za Kilometa tano wanaume Mohammed Gulle wa Arusha
aliibuka kidedea akiwashinda Dotto Ikangaa, pia kutoka Arusha na Pascal
Ramadhan wa Singida.
Mgeni
rasmi katika mbio hizo, ambazo zilishirikisha wanariadha kutoka mikoa
mbalimbalia ya Tanzania na nchi za Kenya , Rwanda Afrika Kusini , Canada na
Australia, alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Liberatus Balo.
Akizungumza
baada ya kukabidhi zawadi, alisema amefurahishwa na juhudi za sekta binafsi
katika kuinua na kuhamasisha michezo nchini na kuomba kampuni nyingi
zaidi zijitokeze kufanya hivyo pia.
"Michezo
inaweza kuwa mojawapo ya vyanzo vya kupata kipato na kusaidia vita
dhidi ya umaskini endapo tu sekta binafsi itajihusisha zaidi
kusaidia kuinua na kupromoti michezo," alisema Balo.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha riadha Tanzania (AT), Suleiman
Nyambui alisema mbio za Rock City Marathon zimeonesha mafanikio
makubwa kadiri miaka inavyosonga mbele.
"Ninajivunia
mbio hizi na nina hakika mustakabali wake ni mzuri mno katika siku
zijazo," alisema Nyambui.
Washindi
wa mbio za kilometa 21 walijinyakulia medali pamoja na
shilingi 500,000 kila mmoja wakati washindi wa pili
waliondoka na shilingi 300,000 kila mmoja na wale walioshika nafasi
ya tatu walizawadiwa shilingi 200,000 huku washindi
wa nafasi ya nne hadi 12 kila mmoja alitapata shilingi 90,000
wakati walioshika nafasi za 13 hadi 50 walipata
shilingi 30,000 kama kifuta jasho.
Washindi
wa mbio za kilometa tano na tatu nao pia walizawadiwa medali pamoja
na fedha taslimu.
Mbio za
Rock City zilizoanzishwa
mwaka 2009 zikiandaliwa na kampuni ya Capital-Plus
International (CPI), inayojishughulisha na masuala mbalimbali ya mawasiliano
yenye makao yake jijini Dar es Salaam zilidhaminiwa na kampuni ya simu za
mkononi ya Airtel, Geita Gold Mine, Shirika la ndege Tanzania
(ATCL), Mfuko wa Pensheni wa Shirika ya Umma (PPF), Bank M, MOIL,
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamiii (NSSF), New Mwanza
Hotel, pamoja na Bodi ya Utalii Tanzania(TTB).
No comments:
Post a Comment