HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 15, 2011

MAKAMU WA RAIS DKT BILAL AKUTANA NA MABALOZI WA UINGEREZA NA BALOZI WA SHIRIKISHO LA UJERUMANI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Balozi wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani , Klaus-Peter Brandes, wakati balozi huyo alipofika kujitambulisha rasmi ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Agot 15.Kushoto ni msaidizi wa Balozi, Haus Koeppel.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani , Klaus-Peter Brandes, wakati balozi huyo alipofika kujitambulisha rasmi ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo .
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Diane Corner, wakati balozi huyo alipomtembelea ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Agot 15. Kushoto ni msaidizi wa Balozi katika Shirika la maendeleo la Uingereza (DFID), Magdalena Banasiak.Picha na Muhidin Sufiani-OMR.

Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal amekutana na Mabalozi wa Uingereza na Ujerumani nchini ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa upatikanaji wa umeme wa kutumia nguvu ya upepo ili kukabiliana na tatizo la umeme hapa nchini.

Mabalozi hao Diane Corner wa Uingereza na Klaus-Peter Brandes wa Ujerumani walipata fursa hiyo ya kuzungumza na Makamu wa Rais walipomtembelea leo Ofisini kwake Ikulu, kwa ajili ya kumsalimia.

Balozi Diane Corner alimweleza Makamu wa Rais kuwa angependa kuona mradi wa umeme wa kutumia nguvu ya upepo ulioko katika mkoa wa Singida unakamilika haraka ili uweze kuanza kutumika mwaka 2013 kama ilivyopangwa.

“Hivi karibuni nilikwenda Singida kuona mradi wa umeme wa kutumia nguvu ya upepo. Ni vizuri mradi huo ukaharakishwe. Huu utakuwa ni mradi wa kwanza kutumia upepo utakapokamilika mwaka 2013. Singida pana upepo mwingi, ni moja ya maeneo pekee kuwa na upepo wa aina hiyo duniani,” alisema Corner.

Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Klaus-Peter Brandes alisema nchi kama Tanzania itajiweka katika nafasi nzuri ya kupiga hatua kimaendeleo endapo itakuwa na umeme wa kutosha ukiwemo na ule unaotokana na nguvu ya upepo.

Akizungumzia mkutano wa Durban kuhusu Mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Disemba mwaka huu nchini Afrika Kusini Balozi Corner alisema Uingereza ina matumaini kuwa mkutano huo utafikia makubaliano ya kisheria ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais alisema Tanzania itahakikisha mradi wa umeme unaotokana na nguvu ya upepo ulioko mkoa wa Singida unakamilika kwa wakati ili kuiwezesha serikali kukabiliana na tatizo la umeme nchini.

Akizungumzia kuhusu mkutano wa Durban Dk. Bilal alisema ni mkutano muhimu kwa kuwa nchi nyingi duniani zikiwemo za Afrika tayari zimeathirika na mabadiliko ya tabianchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad