Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Exim Tanzania wakifanya usafi wa jumla katika kituo cha watoto watukutu ’Jela ya Watoto’ kilichopo Kisutu Dar es Salaam jana.
Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa Benki ya Exim Tanzania wamefanya usafi wa jumla katika kituo cha watoto watukutu ’Jela ya Watoto’ kilichopo Kisutu Dar es Salaam kama sehemu ya ushiriki wa benki hiyo katika mambo ya kijamii nchini.
Meneja Masoko na Uhusiano wa benki hiyo Linda Chiza alisema Dar es Salaam jana kuwa tukio hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki ikiwa ni sehemu ya kijamii kwa benki hiyo lakini pia njia mojawapo ya kuwafariji watoto husika na washauri nasaa wao kuwa watanzania wapo pamoja nao.
Alisema kituo hicho kinajiendesha katika mazingira magumu na kwamba wakati fulani imekuwa ngumu kwa kituo kumudu gharama za mbalimbali za uendeshaji ikiwemo usafi hivyo benki hiyo iliona ni muhimu kwao kusaidia katika kuwapunguzia mzigo.
Chiza alisema pamoja na kuhakikisha kuwa mazingira ya kituo hicho yanakuwa katika hali nzuri kiusafi pia tukio hilo ni njia mojawapo ya kuwaonyesha watoto husika kuwa wazazi wao wapo pamoja nao hivyo hawana budi kubadili tabia.
“Tumekuwa na programu mbalimbali za kijamii hususani katika uwezeshaji lakini sasa tunakwenda mbali zaidi na kuingia katika maisha ya kawaida ya watanzania ambapo leo tumeona tushiriki na wenzetu katika kituo hiki kwa usafi”.
“Taarifa za kituo hiki zinaonyesha kuwa watendaji wana mazingira magumu sana na wakati fulani watoto wamekuwa wakipata mlo mmoja hivyo majukumu mengine yanawazidi uwezo, ndio maana tukaona ni muhimu kwetu kushiriki nao katika usafi ili kuwapunguzia mzigo”, alisema Chiza.
Kwa upande mwingine alisema benki hiyo imekuwa na uhusiano mzuri na kituo hicho ambapo katika sikukuu ya Pasaka mwaka huu walishiriki na watoto husika katika chakula cha pamoja.
Benki ya Exim imekuwa na mchango wa kipekee katika msuala mbalimbali ya kijamii ambapo hivi karibuni imedhamini na kuchangia mfuko maalumu wa Lions Club kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa wa macho nchini.
Pamoja na hayo benki hiyo imekuwa na mikakati na program maalumu za kuiwezesha jamii ya kitanzania katika mambo tofauti hususani upande wa Ujasiriamali kupitia akaunti yake ya Tumaini na program ya WEP kwa wajasiriamali Wanawake.

No comments:
Post a Comment