Wakulima wa tumbaku nchini, kupitia mtandao wa simu wa Airtel, wanao uwezo wa kupata taarifa mazao yao na hivyo kuwawezesha kufanya maamuzi sahii ya mauzo ya mazao yao kupitia simu ya mkononi.
Kuanzia leo, wakulima wataweza kujua bei ya mazao na pembejeo katika muda husika, pesa anazodai na kudaiwa, kwa kupitia mfumo wa AMIS-Connect, ambao umeunganishwa na takwimu za AMIS-Tobacco, mfumo wa mtandao wa kompyuta wenye kuweza kuhifadhi taariza za wakulima.
Mfumo wa AMIS-Connect umezinduliwa leo kwa ushirikiano kati ya CropsData Limited, kampuni inayotoa huduma za kilimo kwa mfumo wa kompyuta, na Airtel Tanzania Limited, kampuni ya mawasiliano yenye viwango vya gharama nafuu. AMIS-Connect ni mfumo wa mawasiliano wa AMIS-Tobacco, mfumo wa usambazaji wa taarifa za kilimo kwa kupitia mtandao wa kompyuta.
Kupitia simu yake ya mkononi, mkulima wa tumbaku nchini anao uwezo wa kujua thamani ya mauzo ya mazao yake tangu awali hadi sasa, kiasi gani anadai katika chama cha ushirika kutokana na mazao aliyopelea na pia kujua anadaiwa kiasi gani kutokana na pembejeo alizochukua. Pia, kupitia simu yake, mkulima anaweza kutazama bei ya pembejeo na zana nyingine za kilimo kulingana na ubora.
Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa kampuni ya CropsData, Charlie Russell, amesema kuwepo kwa huduma hii ya uhakika, uwazi na yenye kutoa taarifa sahihi kutawasaidia wakulima nchini kuweza kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
“Kwa kuwepo mfumo huu wa taarifa tayari utaweza kumlinda mkulima wa tumbaku nchini kuepuka mikono ya wahujumu na walanguzi”, alisema Russell.
Uzinduzi wa mfumo huu umefanyika wakati wa kutano wa wadau wa sekta ya tumbaku kutoka ndani na nje ya nchi, mkutano uliofanyika katika hoteli ya Morogoro.
Akizungumzia uzinduzi wa huduma hii, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Airtel nchini, Beatrice Singano Malya, amesema kwamba kampuni ya Airtel imejidhatiti kuunganisha jamii nzima ya watanzania, wakiwemo wakulima, kwa kuwapatia huduma za mawasiliano ambazo ni nafuu, bunifu na zenye kuleta maana kwao ili kuwawezesha kuhimili mahitaji yao ya kila siku.
Aidha, Malya aliongeza kuwa “Tukiwa kunazidi kueneza mtandao wa mawasiliano yetu katika kila kona ya nchi, tumedhamiria kuwaunganisha wateja wetu wote, hasa wa vijijini, ili kuwaletea maendeleo zaidi ya kiuchumi na kijamii kwenye maeneo yao. Tunaamini kuwa mawasiliano si jambo la anasa bali ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto za maendeleo. Ni kwa sababu hiyo tunajisikia fahari kutoa huduma hii kwa wakulima nchini na hatimaye kuongeza tija katika shughuli zao za kila siku”.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hii, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Injinia Mbogo Mfutakamba, ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya ushirika vinavyojishughulisha na zao la tumbaku nchini kuhakikisha kuwa wanatumia vyema mfumo huu wa AMIS-Connect kwa kushirikiana na Airtel na hatimaye kujiletea maendeleo zaidi.
“Kupitia uzinduzi huu, napenda nisisitize umuhimu wa teknolojia katika uboreshaji wa shughuli za maendeleo. Natumaini huduma bora zitatolewa kwa wanachama sanjari na kuhimili ushindani”, alisema Mfutakamba.
Mwaka 2008, kampuni ya CropsData ilizindua rasmi mfumo wake wa kuhifadhi taarifa za wakulima mkoani Mbeya kwa kushirikiana na Chama Cha Ushirika cha Chunya (CHUTCU). Tangu wakati huo, kila msimu wa kilimo kumekuwepo na ongezeko la vyama vya ushirika vyenye kutumia mfumo wa AMIS-Tobacco kusajili wakulima.
Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku nchini umeruhusu wanunuzi wakuu wa tumbaku nchini (Alliance One, Premium Active na Tanzania Leaf Tobacco) kuweka bayana takwimu zao za ununuzi wa mazao ya wakulima.
Kwa mfumo wa sasa, wanunuaji wa tumbaku nchini wanaweza kutumia njia ya AMIS-Connect kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwenda moja kwa moja kwa wakulima, kuhusiana na taarifa za uzalishaji wa mazao au hata kuwapa taarifa za mafunzo kwa wakulima.
Kwa mujibu wa Malya, mahitaji ya huduma za mawasiliano nchini yamezidi kuongezeka kwa wananchi wa kada mbalimbali na hivyo kufanya kampuni ya Airtel kutathmini na kuja na namna bora ya kuwaletea manufaa zaidi hata wale ambao wako maeneo ya ndani zaidi ya nchi.
Kutokana na mahitaji ya wakulima wa tumbaku nchini, pamoja na yale ya vyama vyao vya ushirika, mtandao wa AMIS-Tobacco umeimarishwa kukidhi mahitaji ya soko kwa wakati huu. Kabla ya kuanza kwa AMIS-Connect, mawasiliano kati ya wakulima na wanunuaji wakubwa wa Tumbaku walitegemea mikutano ya ana-kwa-ana na vyama vyao vya ushirika.
Wadau wa sekta ya tumbaku nchini sasa watategemea zaidi mawasiliano ya simu za mkononi ili kuboresha mfumo wa mawasiliano na usambazaji wa taarifa kwa wakulima hapa nchini.


No comments:
Post a Comment