HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 6, 2011

WADAU WATAKIWA KUTUMIA KEMIKALI RAFIKI KWA MAZINGIRA


Na Riziki Abraham

Wadau wa Mazingira nchini wametakiwa kupunguza ama kutokuzalisha kemikali haribifu ambazo zina athari kubwa kwa mazingira na viumbe hai. Kwa kufanya hivyo watakuwa wametimiza miongoni mwa hatua muhimu katika kutekeleza mkataba wa Stockholm ulioridhiwa mnamo mwaka 2001.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw Twariel Mchome, amesema hayo leo wakati akifungua warsha ya siku mbili jijini Arusha yenye lengo la kukuza ueledi kwa wadau mbalimbali wa mazingira nchini. Amesema hivi sasa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kuweza kukabiliana na tatizo linalotokana na kemikali haribifu kwa mazingira.

Bw.Mchome amebainisha kuwa kemikali hizo zimekuwa zikizalishwa kwa kujua ama kutokujua na wananchi kutokana na shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo, ikiwemo uchomaji taka ovyo, hasa za hopitalini na viwandani kwa kutumia mitambo isiyo bora.

Nae, Mkurugenzi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dr. Julius Ningu, amewataka baadhi ya wafanyabiashara kuongeza uaminifu kwa kuingiza bidhaa zenye ubora unaotakiwa ili kukidhi viwango, hasa kwa kemikali zinazotumika katika shughuli za viwanda, kilimo na hospitali ikiwa ni pamoja na kutokuingiza madawa yaliyopitiliza muda wake.

“Ninasema ni vizuri wafanyabiasha wakaingiza nchini bidhaa zenye viwango vinavyotakiwa hasa kwa upande wa kemikali mbalimbali zinazotumika katika njia za uzalishaji ili kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira nchini” amesema Dr. Ningu.

Aidha, amebainisha madhara mbalimbali ambayo hutokana na uzalishaji wa kemikali hizo unaweza kusababisha magonjwa kama saratani ya ngozi, mabadiliko katika mfumo wa kinga, madhara katika mfumo wa fahamu pamoja na madhara katika mazingira ambayo huathiri hata kiwango cha uzalishaji kutokana na udongo kupoteza ubora wake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi, kutoka ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Bi. Magdalena Mtenga amesema ni vyema wananchi wakatambua kuwa hivi sasa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na baadhi ya Kanuni zipo na zitaanza kuwabana wale wote wanaoingiza ama kutumia kemikali hizi hatarishi, hivyo ni vyema wakafuata sheria na taratibu zinazotakiwa.

Aliongeza kuwa “najua ni kweli baadhi ya kemikali hatarishi bado zinaingizwa nchini lakini kwa kibali maalum mfano matumizi ya kemikali aina ya DDT ambayo bado yanaruhusiwa kuingizwa kutokana na matumizi yake katika nyanja ya utafiti pamoja na matumizi yake katika kuulia mazalia ya mbu nchini”.

Amesema mkataba huu wa Stockholm ulioridhiwa tangu mwaka 2001 unawataka nchi wanachama kupunguza matumizi pamoja na uzalishalishaji wa kemikali hizi haribifu uwe umeshatekelezwa ifikapo mwaka 2025. Kwa kuendelea kutumia njia sahihi zinazoelekezwa na wataalam ikiwa ni pamoja na mfumo sahihi wa kurejeleza taka hizo kutoka viwandani, mahospitalini na katika kilimo.

Warsha hii ya siku mbili yenye lengo la kukuza weledi wa masuala ya kudhibiti kemikali haribifu kwa mazingira na viumbe imeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, ikiwa imeshirikisha wadau mbalimbali kutoka Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro, ambapo ni mwendelezo wa warsha hizi baada ya ile ya awali iliyofanyika jijini Mwanza wiki iliyopita.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad