HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 7, 2011

WADAU WA SEKTA YA SANAA WAOMBA MUSWADA WA HAKIMILIKI UFIKISHWE HARAKA BUNGENI

Mwenyekiti wa Kongamano lililojadili Muswada wa mahuisho ya Sheria ya Hakimiliki na shiriki lililoandaliwa na asasi ya RULU Arts Promotion,Bw.John Kitime (Kulia) akisisitiza jambo wakati akichangia suala la mahuisho ya sheria hiyo.Kulia kwake ni Afisa Kutoka Chama cha Hakimiliki (COSOTA),Doreen Anthony.
Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Idara ya Uchumi Dkt.Aikael J.A akitaja hasara zinazoingiwa na serikali kwa kuchelewesha kuhuisha sheria ya hakimiliki/shiriki ya mwaka 1999.Kulia ni Bw.Kitime.
Msanii Stara Thomas (Kulia) ambaye kwa sasa anaimba muziki wa injili akifuatilia mada kwa makini kwenye kongamano hilo.Kulia kwake ni Mwanasheria wa COSOTA,Moureen.
Msanii wa Muziki wa Reggae Ras Inocent Nganyangwa (aliyevaa kofia) naye alikuwepo kwenye kongamano la kujadili mahuisho ya sheria ya hakimiliki na shiriki.Kushoto kwake Ni Mwandishi wa Tanzania Daima,Makubury Ally na kulia ni moja wa wakurugenzi wa RULU Arts,Ruyembe Mulimba.
Baadhi ya wadau wa kongamano wakifuatilia mjadala kwa makini sana.

Na Mwandishi Maalum

Wadau wa sekta ya sanaa wameiomba Wizara ya Viwanda na Masoko kuharakisha mchakato wa kuipeleka bungeni sheria ya hakimiliki na hakishiriki ili kulinda haki za wasanii ambazo zimekuwa zikiibiwa kwa muda mrefu bila kuwepo udhibiti thabiti.

Wakizungumza kwenye Kongamano la Mapitio ya Marekebisho ya Sheria ya Bunge ya Hakimiliki na shiriki na.7 ya mwaka 1999 lililoandaliwa na Asasi ya RULU Arts Promoters Alhamis wiki hii,wadau walitaka mapendekezo ya mahuisho ya sheria hiyo yaliyowasilishwa wizarani hapo tangu mwaka 2010 yapelekwe haraka bungeni ili haki za wasanii zisiendelee kupotea.

Walisema kwamba,kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Asasi ya RULU ya kufanya utafiti wa eneo hili katika nchi mbalimbali za Afrika na baadaye mapendekezo yake kufikishwa serikalini hakukuwa na sababu ya kusuasua katika mchakato huu kwani kwa kiasi kikubwa ulikuwa umefika kwenye hatua muhimu lakini sasa ni kama umekwama au kurudishwa nyuma.

“RULU arts Promoters kwa udhamini wa shirika la BEST-AC kwa miaka 6 (2006-2011) wamekuwa wakitafuta mbinu za kuifanyia marekebisho sheria ya Hakimiliki na shiriki ya mwaka 1999 kwa lengo la kuwafanya wasanii hasa wanamuziki waweze kupata vipato kulingana na kazi zao na kuzuia mianya ya wizi lakini tunashangaa mchakato wake ni kama hauna kasi” Alisema Bw.Angelo Luhala ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Mafunzo wa Rulu Arts Promoters.

Aliongeza kwamba,Wizara ya Viwanda na Biashara inapaswa kutambua kilio cha wanamuziki nchini hasa cha kuibiwa kazi zao na wao kuishi kwa ufukara mkubwa.

“Wizara itambue kilio cha wanamuziki nchini na kupeleka muswada huu bungeni ili sheria hii ipitishwe haraka sana iwezekanavyo.Itakuwa ni kuendelea kuwadidimiza wasanii wanaojituma sana kwa sasa kama hatutaharakisha mchakato huu” alisisitiza Bw.Luhala.

Kwa upande wake msanii maarufu wa reggae nchini,Inocent Nganyangwa alisema kwamba,kwa ushirikiano wa COSOTA,Kamati kazi maalum iliyoundwa na RULU Arts promoters, kazi kubwa imeshafanyika hivyo wizara haina budi kuupeleka muswada huu mapema iwezekanavyo.

“Kazi kubwa imeshafanyika katika marekebisho ya sheria hii,itakuwa ni kuvunja katiba na sheria za nchi kama tutaendelea kuruhusu sheria iliyopo kuendelea kutumika kwa muda mrefu” alisema Bw.Nganyangwa.

Awali,Doreen Anthony kutoka Chama cha Hakimiliki (COSOTA) alisema kwamba, mahuisho ya sheria hii yako katika hatua nzuri kwani kwa zaidi ya nusu sasa umekwisha kamilika.

Akizungumzia hasara za kuchelewa kupitisha sheria hiyo,Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Dkt.Aikael J.A alisema kwamba,serikali imekuwa ikipoteza mapato mengi sana na zaidi kuifanya sekta ya sanaa kudumaa kwani wasanii wamekuwa hawaoni faida ya kazi zao.

“Tunapaswa kupima athari zinazopatikana sasa,ni lazima kama walivyotangulia kusema wenzangu sheria ipitishwe haraka ili kuwaokoa wasanii na ufukara na kupotea kwa mapato serikalini” alisisitiza Dkt.Aikael.

Suala la wizi wa kazi za wasanii hapa nchini ni kilio cha muda mrefu sasa na hali inakuwa mbaya zaidi pale vijana wengi wanapojiajiri huko na kukosa mkakati madhubuti wa kisheria wa kulinda haki zao

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad