Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni Prof.Hermans Mwansoko(kulia) akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo juu ya maadhimisho ya siku ya utamaduni kitaifa yanayotarajia kufanyika mkoani Mara kuanzia 19.5.2011 hadi 21.5.2011. wengine katika picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo Bw.Sethi Kamuhanda (katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Mara Luteni mstaafu, Enos Mfuru (kushoto)
Na Concilia Niyibitanga- Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Serikali iliamua Siku kuu ya Utamaduni Duniani iwe inaadhimishwa mikoani kwa zamu ili wananchi wote wapate haki na fursa ya kujifunza zaidi kuhusu utamaduni wao, kutambua tofauti za tamaduni mbalimbali, kuziheshimu, kuzithamini, kuzienzi na kushiriki katika kudumisha na kuendeleza utamduni wao.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Bw. Sethi Kamuhanda wakati akiongea na Wandishi wa Habari kuhusu Siku ya Utamaduni Duniani inayotarajia kuadhimishwa Kitaifa Mjini Musoma Mkoani Mara kuanzia tarehe 19-21 Mei, 2011.
Bw. Kamuhanda alisema kuwa Kaulimbiu ya Siku ya Utamaduni mwaka huu ni ‘Tusherehekeapo Miaka 50 ya Uhuru, Tudumishe Utamaduni Wetu’. Alisema kuwa kaulimbiu hii inalenga kuhimiza Wananchi, kuendelea kuenzi na kudumisha amani, utulivu na mshikamano ambao umejengwa na utamaduni wao wa kupendana.
Bw. Kamuhanda alisema kuwa katika maadhimisho hayo kutakuwa na maonyesho ya shughuli mbalimbali za utamaduni zikiwemo sanaa za maonyesho kama vile ngoma za asili, maigizo, majigambo, sarakasi na ngonjera.
Aidha, alisema kuwa kutakuwa na sanaa za ufundi kama vile uchoraji, uchongaji, ususi, uhunzi, ufumaji, ushonaji na mavazi, uchongaji, mapishi ya vyakula vya asili na ufinyanzi.
Kutakuwa pia na maonyesho ya muziki ikiwa ni pamoja na muziki wa asili, muziki wa kizazi kipya, taarabu na dansi. Aliongeza Bw. Kamuhanda.
Alisema kuwa kutakuwa na Monyesho ya Filamu zilizokaguliwa na Bodi ya Filamu na kutakuwepo na michezo ya jadi kama vile mieleka, bao, kulenga shabaha, kuvuta kamba, mbio za gunia, kufukuza kuku na mdako.
Kwa upande wa Lugha kutakuwa na kutunga na kughani mashairi, tenzi, ngonjera na hadithi pia kutakuwa na maonyesho ya vitabu. Alieleza Bw. Kamuhanda.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mstaafu Bw. Enos Mafuru alisema kuwa mkoa wake umeshajipanga na alitoa wito kwa Wanahabari kuwatangazia wananchi kushiriki katika sherehe hizo.
Mwaka 2002 Umoja wa Mataifa uliamua kuanzisha maadhimisho ya siku ya Utamaduni Duniani kutokana na kuongezeka kwa migogoro, mapigano na kupotea kwa maisha ya watu na mali zao iliyokuwa inatokea sehemu mbalimbali duniani mwishoni mwa miaka ya 1990.
Inaaminika kuwa chanzo cha migogoro hiyo ilikuwa ni kutofautiana kwa tamaduni ambako kunaleta kugawanyika na kuacha kushirikiana na kuingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
No comments:
Post a Comment