HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 19, 2010

MKUTANO MKUU WA SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII


Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inatarajia kuendesha Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii katika Ukumbi wa Mount Uluguru, Mkoani Morogoro kuanzia tarehe 22-24 Novemba, 2010.

Madhumuni ya Mkutano huu ambao unafanyika kila mwaka, una lengo la kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya Maendeleo ya Jamii hapa nchini kuweza kubadilishana uzoefu wa utendaji kazi, kupima matokeo ya utekelezaji wa majukumu yao na kutafakari mbinu za kukabiliana na changamoto za kisekta katika kuhamasisha jamii kujiletea maendeleo endelevu. Mkutano huu unawashirikisha wataalamu mbalimbali katika nyanja zote wanaojihusisha na maendeleo ya jamii kwa ujumla ikizingatiwa kwamba sekta hii ni mtambuka.

Kila mwaka, Wizara imekuwa ikiandaa Mkutano wa Kisekta kwa kuwa na kaulimbiu mahsusi kulingana na vipaumbele vya maendeleo kwa wakati huo. Mwaka 2010 kaulimbiu, ni

“USHIRIKI WA JAMII NA USAWA WA JINSIA: MSINGI WA MAENDELEO ENDELEVU”. Kaulimbiu hii imeandaliwa mahsusi kwa kuzingatia umuhimu wake katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara, Sekta ya Maendeleo ya Jamii na malengo ya Taifa kwa ujumla. Ni dhahiri kwamba jamii inapozingatia usawa wa jinsia na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, kunakuwepo na maendeleo endelevu.

Tafiti mbalimbali na mapitio ya mikakati na sera za jumla, mfano MKUKUTA, zinaonesha kuwa jitihada kubwa zinazoelekezwa katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa sehemu kubwa hazijazingatia mahitaji muhimu ya wanawake na wanaume katika jamii na ndiyo maana matokeo ya kukua kwa uchumi hakuoneshi picha halisi ya usawa wa jinsia.

Aidha, wakati wa Mkutano huu mada mbalimbali zitawasilishwa kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu. Mada hizo ni pamoja na: Mchango wa Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kuwezesha maendeleo kwenye Halmashauri na changamoto zinazowakabili; Mchango wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii katika kufanikisha Kilimo Kwanza; kutekeleza Dira ya Taifa ya ya Maendeleo, Malengo ya Sera za Jumla mfano MKUKUTA, malengo ya sera mbalimbali ikiwa ni pamoja na Malengo ya millennia.

Washiriki wa Mkutano huu wanatarajiwa kutoka Wizarani, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na vile vya Maendeleo ya Wananchi, Washauri wa Maendeleo ya Jamii katika Sekretarieti za Mikoa, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri zote za jiji, Manispaa, Miji na Wilaya. Aidha, Mkutano utashirikisha wawakilishi kutoka katika Wizara nyingine na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, Mkutano huo utafunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Issa Saleh Machibya.


Hafsa S. A. Duduma

KAIMU KATIBU MKUU

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad