HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 12, 2010

Jeshi La Polisi Kupiga Mnada Magari Yake Mabovu


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi

Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi nchini kufanya uratatibu wa kuyapiga mnada magari yote mabovu ya Jeshi hilo ili kupunguza matumizi ya kuyahudumia ama kuongeza uharibifu wa mazingira katika maeneo ya vituo vya Polisi.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Hazina Bw. Ramadhani Khijjah,

wakati akipokea taarifa ya Timu maalum ya Wataalamu wa Masuala ya Uchumi kutoka Jeshi la Polisi na Wizara ya Fedha iliyotathimini mahitaji ya kibajeti ya Jeshi la Polisi nchini.

Amesema uzoefu umeonekana kuwa magari mengi ya Jeshi la Polisi yanayoharibika, yamekuwa yakirundikana kwenye vituo na Karakana mbalimbali za Jeshi hilo hapa nchini bila ya kuwepo kwa utaratibu unaobainishwa wa kuyauza magari ya Serikali. Hata hivyo Bw. Khijjah ameshauri kuwa fedha zitokanazo na mauzo ya magari hayo zinaweza pia kutumika moja kwa moja kwenye miradi mbalimbali ya Jeshi la Polisi.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo ameishauri Wizara ya Mambo ya Ndani, kuharakisha mchakato wa utungwaji wa Sheria inayoyahusu makampuni binafsi ya ulinzi hapa nchini ili askari wa Makampuni hayo wafanye kazi kwa kuzingatia ubora wa huduma ya ulinzi na kuepuka walinzi hao kujihusisha na vitendo vya kihalifu. Bw. Khijjah amesema kwa siku za hivi karibuni kumekuwapo na taarifa za matishio ya baadhi ya walinzi wa makampuni binafsi kujihusisha na vitendo vya uhalifu katika maeneo ya malindo yao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Ndani Bw. Mbaraka Abdulluwakili, amesema kuwa sheria ipo mbioni na kwamba wakati mchakato wake ukiendelea, hivi sasa Jeshi la Polisi nchini linaendelea kutoa elimu kwa askari wa makampuni mbalimbali ya ulinzi ili wawe na maadili mema.

Akizungumza katika mkutano huo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, amesema kuwa ushirikishwaji wa Makampuni binafsi ya ulinzi katika masuala ya kiusalama kutasaidia kupunguza uhalifu hapa nchini.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa bidhaa ya usalama, Jeshi la Polisi limeazimia kuendelea kutoa elimu ya ukamataji salama na mpango wa Polisi Jamii na ulinzi shirikishi. Wakati huo huo Kampuni ya Sigara nchini TCC imesema itaendeleza utaratibu wake wa kugharimia safari za mafunzo ya nje ya nchi kwa Viongozi wa Jeshi la Polisi mpango ambao ulianza miaka minane iliyopita. Ahadi hiyo, imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Kampuni ya Sigara nchini Bw Frank Usiri, wakati akizungumza na Maafisa wa Juu wa Jeshi la Polisi Jijini Dar es Salaam.

Bw Usiri amesema kuwa utaratibu huo ulianzishwa tangu mwaka 2002 enzi za uongozi wa Inspekta Jenerali Mstaafu Omari Mahita, ambapo amesema hadi sasa Kampuni hiyo imeshatumia zaidi ya Dolla za Marekani 800,000 kwa Maafisa Wakuu kushiriki katika mikutano ya Kimataifa sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 1.1.

Naye Meneja Usalama wa Kampuni hiyo Bw. Issa Massare, amesema kuwa ushirikiano uliopo baina ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Sigara nchini umesaidia kubaini sigara feki zinazoonyesha kuwa zimetengenezwa na Kiwanda cha Sigara nchini TCC jambo ambalo sio la kweli.

Amesema Kampuni ya Sigara nchini TCC ina mpango wa kutawanya vifaa vya kiusalama kwa Jeshi la Polisi vitakavyosaidia kubaini fedha bandia na bidhaa za viwandani zilizoghushiwa

1 comment:

  1. HII IKISHA PIGA MNADA WALIONUNUWA WAKIAANZA NAYO BARABARANI WANAWAKAMATA KWAMBA NI MABOVU SASA SI ZULUMA HIZO? PAzi.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad