HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 6, 2009

mabomu yaliyosalia huko mbagala,kulipuliwa kesho

mabaki ya mabomu yaliyolipuka siku za hivi karibuni huko Mbagala.

Kesho kuanzia saa tisa alasiri Jeshi la Wananchi litalipua masalia ya mabomu yaliyobaki katika ghala la jeshi hilo katika kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), 671 Mbagala kuepusha uwezekano wa mabaki hayo kuleta madhara zaidi.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi amesema leo kwamba kazi hiyo itafanywa na wataalamu wa Jeshi na hakutakuwa na madhara yeyote kwa watu kwani yatalipuliwa kiufundi.
Lakini alisema watu itabidi kuanzia muda huo wakae mita 500 kutoka eneo la Kambi hiyo.

Kiasi cha watu 25 wamepoteza maisha yao katika mlipuko huo wa mabomu uliotokea wiki iliyopita, na mamia walijeruhiwa. Takriban watoto 200 walipotezana na familia zao, ingawa hivi sasa karibu wote wamerudi makwao.

Mh. Mwinyi amesema wananchi wasiwe na wasiwasi kwani zoezi hilo litafanyika kwa umakini. Amesema kwanza kabisa kutakuwa na milipuko miwili midogo kwa ajili ya kutoa tahadhari. Baada ya hapo amesema itafuatia milipuko mingine ya mfululizo ya nguvu kiasi hadi saa 11 jion.

Mh. Waziri wamewaomba wananchi waondokea maeneo hayo na kuwa umbali wa mita 500 kutoka kambi ya Mbagala na kusisitiza kwamba wananchi wasiwe na hofu kwani zoezi litaendeshwa kwa utaalamu. Silaha zitakazoharibiwa ni pamoja na masalia ya risasi, baruti, viwashio na mabomu ambayo hayakuweza kulipuka siku ilipotokea ajali.

Mh. Mwinyi amesema mabomu 75 ya kutupa kwa mkono aina ya Stick hand grenades na dazeni kadhaa za viwashio pamoja na fyuzi zake zitateketezwa. Alisema mabomu hayo inabidi yaharibiwe eneo hilo kwa sababu yanaweza kulipuka wakati wa kuyahamisha na kuleta madhara kwa watu watakao yahamisha.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Lukuvi alisema wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida kwani zoezi hilo halitaweza kuingilia kazi za watu.

Lukuvi alisema hata wanafunzi waendelee kwenda shule kama kawaida na kusitokee kisingizio chochote cha wanafunzi au watu kushindwa kwenda kwenye shughuli zao au shuleni.

Naye Mkuu wa Usalama wa JWTZ, Brigedia Generali Paul Mella alisema kambi ya Mbagala ina wanajeshi 200 ambao watasaidia kuwaelekeza wananchi kabla ya ulipuaji wa mabomu kuanza.habari kwa msaada wa Michuzi Blog

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad