HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 23, 2026

WAZIRI: SEKTA BINAFSI NI NGUZO MUHIMU KUTEKELEZA DIRA 2050

 



NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Leonardo Akwilapo, amesema sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika usimamizi wa ardhi, uendelezaji wa miji ya kisasa, makazi bora na ukuaji wa uchumi.

Akizungumza Novemba 11, 2026, jijini Dar es Salaam, katika kikao kazi na kampuni za upangaji, upimaji na uendelezaji wa milki, Waziri huyo amesema ardhi ni rasilimali muhimu inayobeba shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, viwanda, ujenzi wa nyumba, ofisi na uwekezaji wa biashara.

Amesema Dira ya Taifa ya 2050 imeipa sekta ya ardhi nafasi muhimu kutokana na uwezo wake wa kuchochea maendeleo ya wananchi na kufikia malengo ya uchumi, hivyo ni lazima kuweka mifumo imara ya usimamizi na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi.

Waziri amesema serikali haiwezi kutekeleza Dira ya 2050 peke yake, kwa kuwa sekta binafsi imepewa nafasi kubwa katika kuchochea shughuli za kiuchumi, hivyo ni muhimu kushirikiana katika ubunifu wa miji ya kisasa, ujenzi wa makazi ya gharama nafuu, kuboresha makazi yaliyopo na kuimarisha usalama wa milki.

Amesema ushirikiano huo unapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kitaaluma, huku akisisitiza kuwa serikali na sekta binafsi ni washirika wanaojenga nyumba moja na wanapaswa kuzungumza kwa uwazi, kukosoana na kutatua changamoto kwa lengo la kuleta maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri amesema serikali ipo katika maandalizi ya kuanzisha Mamlaka ya kusimamia sekta ya milki nchini, ambayo itakuwa na nguvu za kisheria za kuratibu na kusimamia shughuli za sekta hiyo, akieleza kuwa muswada wake unatarajiwa kuwasilishwa Bungeni katika nusu ya pili ya mwaka 2027 baada ya kukamilisha hatua za mashauriano na wadau.

Amesema kuanzishwa kwa mamlaka hiyo kutasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki, kudhibiti ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma, udanganyifu na migogoro ya ardhi, pamoja na kuweka mfumo wa pamoja wa utendaji kwa wadau wanaohusika.

Aidha, amesema serikali inaendelea na programu ya urasimishaji wa makazi yaliyopangwa kiholela na kuzuia uanzishwaji wa makazi mapya yasiyozingatia mipango miji, akibainisha kuwa changamoto ya makazi yasiyopangwa imeendelea kuathiri mandhari ya miji, upatikanaji wa huduma na maendeleo endelevu.

Waziri ametoa rai kwa sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kuboresha makazi chakavu na kuhuisha maeneo ya mijini yenye thamani kubwa, bila kuathiri haki za wananchi katika maeneo yao, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia mipango miji na matumizi sahihi ya ardhi.

Ameongeza kuwa serikali pia inafuatilia changamoto za ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi, baada ya kubainika kuwa baadhi ya wananchi wanaotaka kulipa wanakabiliwa na vikwazo vya kupata namba za malipo, akielekeza uchunguzi kubaini kama tatizo linatokana na mifumo ya kiteknolojia, watendaji au sababu nyingine.

Waziri amesema sekta ya milki ina mchango wa takribani asilimia 4.4 katika Pato la Taifa, hivyo kuna haja ya kuimarisha usimamizi wake ili kuongeza mapato ya serikali, kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi, huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na mazingira bora ya kufanya kazi.

Pia amesema kwamba Serikali inathamini mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya ardhi, milki na makazi nchini, na kwamba ushirikiano wa karibu, uwazi, uwajibikaji na kuzingatia taaluma ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad