
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano na ushirikiano na wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo, ikieleza kuwa uhusiano mzuri kati ya pande hizo ni nguzo muhimu katika kujenga mazingira bora ya biashara na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Wito huo umetolewa na Kamishna wa Kodi za Ndani, Eva Raphael Magoti, akizungumza katika hitimisho la maombolezo ya aliyekuwa mfanyabiashara wa Kariakoo na Mwenyekiti wa Kijiwe cha Raha Square, Marehemu Rweyemamu Erasto, ambapo viongozi wa TRA na wafanyabiashara walishiriki kumuaga.
Magoti amesema TRA haitakiwi kuhusishwa na wafanyabiashara katika masuala ya kodi pekee, bali inapaswa kuwa na mahusiano ya karibu nao katika shughuli mbalimbali za kijamii ili kujenga mshikamano na kuimarisha ushirikiano.
Amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara katika masuala yenye maslahi kwa jamii, akisisitiza kuwa kujenga Taifa kunahitaji hiari, umoja na mahusiano mazuri baina ya taasisi na wananchi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kariakoo, Haji Manara, amewataka wafanyabiashara kuendeleza ushirikiano na TRA, akieleza kuwa mahusiano mazuri yaliyopo yamechangia Mkoa wa Kikodi Kariakoo kufanya vizuri na kuwa kinara katika ukusanyaji wa mapato.
Manara amesema ushirikiano huo umesaidia kutatua kwa haraka changamoto mbalimbali za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara, huku akiwataka kuendeleza mchango na kazi nzuri zilizoachwa na marehemu Rweyemamu katika kuwakilisha maslahi yao.
Uongozi wa TRA kupitia Kamishna wa Kodi za Ndani umetoa mchango kiasi cha Shilingi Milioni Mbili (2,000,000/=) ikiwa ni kwa ajili ya maulid ya kuombea soko la Kariakoo lililopangwa kufanyika Novemba 29, 2026 na Diwani wa Kariakoo Haji Manara
Aidha, Manara amewaalika viongozi wa TRA na wafanyabiashara wa Kariakoo kushiriki Maulid maalum ya kuliombea Soko la Kariakoo, yatakayofanyika Jumapili, Novemba 29, 2026, katika Soko Jipya la Kariakoo.


.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

No comments:
Post a Comment