Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania imeelekeza nguvu katika kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali kupitia huduma ya M-Pesa wakati wa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, huku ikiandaa zawadi mbalimbali kwa wateja wake zikiwemo magari matano mapya aina ya Jetour.
Kupitia kampeni ya “Zaidi ya Malipo, Ni Shangwe”, Vodacom inalenga kuhamasisha Watanzania kutumia njia za kidijitali katika kufanya malipo ya bidhaa na huduma mbalimbali, badala ya kutegemea fedha taslimu katika shughuli zao za kila siku.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania, Brigita Shirima, amesema kampuni hiyo imeandaa kampeni hiyo kwa lengo la kuendelea kuwahudumia wateja wake na kukidhi mahitaji yao katika kipindi cha sikukuu.
Amesema matumizi ya M-Pesa yanawawezesha wananchi kufanya miamala kwa urahisi kupitia simu zao wanapofanya manunuzi, kujaza mafuta, kula migahawani na kulipia huduma nyingine bila ulazima wa kubeba fedha nyingi taslimu.
Ameongeza kuwa wateja watakaotumia M-Pesa kufanya malipo katika kipindi cha kampeni hiyo watapata nafasi ya kushiriki droo za kujishindia zawadi mbalimbali, zikiwemo magari matano aina ya Jetour pamoja na simu za mkononi.
Baadhi ya zawadi hizo zimeoneshwa katika hafla ya Vodacom Shangwe Festival, ikiwa ni sehemu ya utambulisho wa kampeni hiyo inayochanganya hamasa ya matumizi ya malipo ya kidijitali na fursa za zawadi kwa wateja.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, amesema msimu wa sikukuu ni fursa muhimu ya kujenga utamaduni wa matumizi ya malipo ya kidijitali, hasa kipindi ambacho shughuli za ununuzi, safari na sherehe huongezeka na kusababisha mzunguko mkubwa wa fedha taslimu.
Amesema matumizi ya fedha taslimu yanaweza kuambatana na changamoto za wizi, upotevu wa fedha, foleni na ukosefu wa chenji katika maeneo ya biashara, hivyo matumizi ya teknolojia ya kifedha yanaweza kusaidia kurahisisha shughuli hizo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa, Tulisindo Mlupilo, amesema lengo ni kuhakikisha malipo ya kidijitali yanakuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya wananchi, badala ya kutumika katika vipindi maalumu pekee.
Ameeleza kuwa wateja wanaweza kufanya malipo kupitia QR Code, namba za Lipa na kadi ya M-Pesa Visa katika maduka makubwa, vituo vya mafuta, migahawa na maeneo mengine ya biashara.
Huduma hizo pia zinatumika katika ununuzi wa muda wa maongezi na vifurushi, ulipaji wa bili pamoja na baadhi ya huduma za usafiri zinazohusisha mabasi, treni ya SGR na ndege.
Kampeni hiyo inaendana na juhudi za kuimarisha uchumi unaopunguza matumizi ya fedha taslimu, huku ikiwapa wananchi fursa ya kutumia teknolojia katika malipo yao ya kawaida bila kulazimika kubadilisha namna wanavyonunua au kuongeza matumizi yao.

No comments:
Post a Comment