HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, November 28, 2026

JUNEID OTHMAN ATWAA TUZO YA MKURUGENZI BORA KIJANA

 Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mkuyu Africa, Juneid Othman, ametwaa tuzo ya Mkurugenzi Bora Kijana (Future Executive to Watch) katika tuzo za Top 100 Executive Awards zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Tuzo hizo zilitanguliwa na mkutano wa siku mbili uliowakutanisha wakurugenzi wa kampuni mbalimbali kutoka barani Afrika, kwa lengo la kujengeana uwezo, kubadilishana uzoefu na kujadili fursa za uwekezaji zilizopo katika nchi zao.

Miongoni mwa washiriki wa mkutano huo walitoka Nigeria, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Juneid amesema mafanikio aliyoyafikia yametokana na juhudi zake binafsi pamoja na mchango wa watu wanaomzunguka katika shughuli za biashara.

Amesema anaitoa tuzo hiyo kwa wafanyakazi wa kampuni yake, ambao wengi wao ni vijana, akieleza kuwa wamekuwa msaada mkubwa katika safari yake ya ujasiriamali kupitia ushauri, ushirikiano na mawazo yao katika kukuza biashara.

Juneid anaiongoza kampuni ya Mkuyu Africa inayojihusisha na shughuli za ujenzi, ununuzi na uuzaji wa nyumba na viwanja pamoja na upangishaji wa nyumba za makazi katika maeneo ya Kariakoo, Masaki na Kawe jijini Dar es Salaam, ambako kampuni hiyo ina miradi mbalimbali ya biashara na makazi.

Amesema ana malengo ya kutekeleza miradi isiyopungua 3,000 ifikapo mwaka 2030, hatua ambayo amesema inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2030.

Ameeleza kuwa kutunukiwa tuzo hiyo ni hatua muhimu katika safari yake ya uongozi na ujasiriamali, huku akihimiza Watanzania kutambua fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kushiriki katika umiliki wa mali na kutokuwa na hofu ya kuwekeza ndani ya nchi.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya nchi yanahitaji ushiriki wa wananchi wenyewe kupitia uwekezaji na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Mkuyu Africa imeingia makubaliano ya kibiashara na kampuni ya DAMAC ya nchini Dubai inayojihusisha na uuzaji na upangishaji wa majengo, hatua inayotarajiwa kurahisisha upatikanaji wa fursa za uwekezaji wa majengo nchini humo kwa Watanzania wanaotaka kuwekeza Dubai.
Mkurugeni wa kampuni ya MKUYU Africa Juneid Othman(kushoto) akipokea Tuzo ya mkurugenzi bora kijana (Future Exacutive to Watch) wakati wa tuzo za Top 100 Executive Award zilizofanyika jijini Dar Salam





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad