
KAIMU Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Athumani Kilundumya,
amesema kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Azimio la Kampala chini ya Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Kilimo Barani Afrika (CAADP), kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula, kukuza ajira na kuongeza mchango wa Sekta ya Kilimo katika uchumi wa Taifa.
Akizungumza wakati wa hitimisho la Ziara ya Uhamasishaji wa Utekelezaji wa Azimio la Kampala, tarehe 20 Novemba 2026 katika Hoteli ya Best Western jijini Dodoma, Mhandisi Kilundumya amesisitiza kuwa azimio hilo linaendana na vipaumbele vya Serikali vya kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo kupitia sera, mikakati na uwekezaji unaolenga kuongeza tija na ushindani wa mazao ya kilimo.
Mhandisi Kilundumya, ambaye amemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amewashukuru wajumbe kutoka Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Sekretarieti ya SADC, Serikali ya Sudan Kusini, Wizara mbalimbali za Serikali, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali pamoja na Wadau wa Maendeleo kwa ushirikiano na michango yao iliyochangia mafanikio ya ziara hiyo.
Alieleza kuwa ziara hiyo imeongeza uelewa kuhusu malengo ya Azimio la Kampala na kutoa fursa kwa wadau kujadili hatua za kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya mageuzi ya kilimo inayolenga uzalishaji wenye tija, biashara ya mazao, maendeleo ya viwanda vinavyotegemea kilimo, pamoja na kuimarisha mifumo himilivu ya chakula na lishe.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza agenda ya CAADP kwa kuimarisha uwekezaji katika umwagiliaji, matumizi ya zana na teknolojia za kisasa za kilimo, upatikanaji wa masoko na huduma za ugani, hatua ambazo ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo na ustawi wa wananchi.
Azimio la Kampala linatoa dira mpya ya maendeleo ya kilimo barani Afrika kwa kuhimiza nchi wanachama kuongeza kasi ya mageuzi ya Sekta hiyo ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, kuhakikisha usalama wa chakula na kujenga mifumo endelevu ya uzalishaji wa kilimo inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
No comments:
Post a Comment