HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 16, 2026

Tanzania Yageukia Vyakula vya Asili Kudhibiti Magonjwa Sugu

 


Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
TANZANIA imeweka wazi utayari wake wa kufanya tafiti za kina, kuhifadhi kumbukumbu za vyakula vya asili na kuzitumia kukabiliana na wimbi linalozidi kushika kasi la magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), wataalamu wa afya walieleza jana.

Akizungumza wakati akifungua kongamano la kisayansi la Mpango wa Lishe Duniani (World Diet Initiative) jijini Dar es Salaam, leo Novemba 16, 2026 Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya, alionya kuwa nchi inakabiliwa na changamoto pacha za lishe zinazotishia afya ya jamii na uchumi wa taifa.

Kongamano hilo la kimataifa, lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), limewakutanisha wanasayansi wabobezi, watunga sera, na wataalamu wa afya ya jamii kutoka zaidi ya mataifa 16.

Profesa Sunguya alitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni Uholanzi, Marekani, Brazil, India, na Romania, akieleza kuwa jukwaa hilo linalenga kuchunguza kwa kina namna mifumo ya vyakula vya asili inavyoimarisha kinga ya mwili na kukinga dhidi ya maradhi sugu.

Alifafanua kuwa wakati tatizo la udumavu na upungufu wa virutubisho muhimu vikiendelea kuwepo, viwango vya uzito uliopitiliza, unene uliokithiri, na magonjwa yanayochochewa na mtindo wa maisha kama vile shinikizo la juu la damu, kisukari, na magonjwa ya moyo—vinaongezeka kwa kasi, hali inayoelemea familia na mfumo wa afya nchini.

"Changamoto hizi zinatupasa kwenda mbali zaidi ya tiba ya magonjwa na kuelekeza nguvu kwenye viini vya tatizo, ikiwemo ulaji usiofaa na mabadiliko ya mazingira ya chakula," Profesa Sunguya aliwaambia washiriki, akisisitiza kuwa lishe bora ni nguzo muhimu ya maendeleo na usalama wa taifa.

Hata hivyo, alitahadharisha kuwa vyakula vya asili havitoi kinga dhidi ya maradhi moja kwa moja, akihimiza umuhimu wa kufanyika kwa tafiti za kina za kisayansi kuhusu virutubisho vilivyomo, mbinu za uandaaji, na uwiano sahihi wa mlo kabla ya kuvijumuisha kwenye sera rasmi za afya ya umma.
Akiunga mkono hoja hiyo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha MUHAS, Profesa Sabina Mugusi, alisema ukuaji wa kasi wa miji, utandawazi, na ongezeko la vyakula vilivyosindikwa viwandani vinabadilisha kwa haraka mfumo wa ulaji nchini.

Aliwahimiza watafiti kuziba pengo kati ya tafiti na jamii kwa kubadilisha matokeo ya maabara kuwa suluhu za vitendo, zinazoendana na utamaduni wa wenyeji na zenye gharama nafuu.

Mwanazuoni huyo aliongeza kuwa wajumbe wa kongamano hilo wanalenga kuweka ajenda ya pamoja ya utafiti wa kimataifa ili kulinda urithi wa mapishi unaotoweka na kuongoza mikakati endelevu ya lishe barani Afrika na kwingineko.
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha KCMC, Dk. Godfrey Temba, alisema matokeo ya awali ya utafiti wa miaka saba uliofanyika mkoani Kilimanjaro yanaonyesha kuwa vyakula vikuu vya asili vina uwezo mkubwa wa kulinda afya.

Dk. Temba alibainisha kuwa vyakula vya asili kama vile kiburu—mlo unaoandaliwa kwa mchanganyiko wa maharage na ndizi—pamoja na mazao ya mizizi na kinywaji cha asili cha mbege kinachotengenezwa kwa kuchachusha ulezi na ndizi, vina vimelea hai vyenye manufaa na virutubisho muhimu vinavyoimarisha kinga ya mwili na kupunguza hatari ya magonjwa sugu bila kutumia kemikali zozote.









No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad