HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, November 16, 2026

HOMERA AZITAKA TAASISI ZA MAFUTA NA GESI KUNUFAISHA SERIKALI NA WATAALAMU WAKE

 


Na Mwandishi Were
WAZIRI wa Nishati Dkt.Juma Homera, amezitaka taasisi za umma zinazohusika na sekta ya mafuta na gesi kuhakikisha wataalamu wanaopelekwa mafunzoni kwa kutumia fedha za umma wanabaki katika utumishi wa Serikali kwa muda wa kutosha ili waweze kuhamisha ujuzi walioupata na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Amesema Serikali inawekeza katika kujenga uwezo wa wataalamu wazawa ili kuwaandaa Watanzania kunufaika na fursa zinazotokana na kukua kwa sekta ya mafuta na gesi, akionya kuwa uwekezaji huo unaweza kukosa tija endapo wataalamu wanaofadhiliwa wataondoka mara moja kwenda kufanya kazi katika sekta binafsi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), uliofanyika jijini Dar es Salaam Dkt. Homera alisema programu za mafunzo zinapaswa kwenda sambamba na makubaliano ya wazi ya wanufaika kuitumikia nchi.

" Mafunzo yanapaswa kuwanufaisha Watanzania. Tunapowagharamia wataalamu wetu kupata ujuzi maalumu, wanapaswa kurejea na kutumia ujuzi huo kuwatumikia Watanzania kabla ya kufikiria fursa nyingine nje ya Serikali," alisema.

Aliongeza kuwa Serikali itashirikiana na PURA kutafuta rasilimali kwa ajili ya kuwaendeleza watumishi wake kitaaluma, hususan wakati Tanzania ikijiandaa kutekeleza miradi mikubwa ya mafuta na gesi itakayohitaji wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu.

Kauli ya Waziri huyo inakuja wakati Tanzania ikiimarisha juhudi za kupanua shughuli za utafutaji wa mafuta, kuendeleza rasilimali za gesi asilia na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika sekta ya petroli.

Dkt.Homera pia aliwataka watumishi wa PURA kuzingatia nidhamu, uwazi, weledi na uwajibikaji, akisema usimamizi bora wa rasilimali za umma ni muhimu katika kuhakikisha nchi inanufaika na utajiri wake wa asili.

Alionya watumishi dhidi ya kutoa taarifa nyeti za Serikali na miradi kabla ya maamuzi na taratibu rasmi kukamilika, akisema kufanya hivyo mapema kunaweza kuathiri maslahi ya Taifa na kuwapa washindani fursa ya kupata manufaa yasiyostahili.

"Msikimbilie kutoa taarifa za kimkakati kabla Serikali haijakamilisha taratibu zinazohitajika. Tunapaswa kulinda taarifa zinazoweza kuathiri maslahi ya Taifa, huku tukihakikisha Watanzania wanaelewa fursa na manufaa yaliyopo katika sekta hii," alisema Dkt.Homera.

Kuhusu ushiriki wa wazawa, Homera aliipongeza PURA kwa mchango wake katika kupanua fursa kwa kampuni na wataalamu wa Kitanzania kushiriki katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi.

Alisema sekta hiyo imezalisha ajira kwa Watanzania wapatao 350, huku kampuni za ndani zikifanikiwa kupata zabuni za ununuzi wa bidhaa na huduma zenye thamani ya takribani Sh bilioni 20.

Aidha, aliipongeza PURA na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa mchango wao katika kuimarisha uwezo wa kitaalamu wa nchi kwenye shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi.

Alitaja hatua ya kutolewa kwa leseni nne za utafutaji kwa kushirikiana na TPDC kuwa ni maendeleo muhimu katika kujenga utaalamu wa ndani na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.

Pia alizungumzia maandalizi yanayoendelea kwa ajili ya kuendelezwa kwa mradi wa gesi asilia wa Ntorya mkoani Mtwara, ambao unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa gesi nchini na kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Charles Sagweni, alisema Mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha usimamizi na udhibiti wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli, hususan utafutaji, uendelezaji wa gesi asilia, ushiriki wa wazawa na uzingatiaji wa sheria na kanuni za petroli.

Alisema maeneo hayo yanaongeza fursa za uwezekano wa kugunduliwa kwa rasilimali mpya za petroli nchini.

Sagweni alisema Mamlaka hiyo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza shughuli za utafutaji, ikiwemo maandalizi ya kuchimba kisima cha utafutaji wa mafuta na gesi.

Alifafanua kuwa zaidi ya kampuni 10 za Kitanzania zimefanikiwa kupata mikataba katika kampeni za hivi karibuni za utafutaji, huku Watanzania wapatao 320 wakipata ajira za muda na za kudumu.

Alisema PURA pia imeshiriki katika mapitio ya kanuni za sekta ya petroli, ambapo Kanuni za Petroli zimechapishwa katika Gazeti la Serikali.

Aidha, rasimu za kanuni zinazohusu shughuli za Kamisheni ya Petroli, ushiriki wa wazawa na uwajibikaji kwa jamii zimewasilishwa katika Wizara ya Nishati kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi.

Hata hivyo, Sagweni alitaja changamoto zinazohusiana na utekelezaji wa kanuni za fedha za kigeni, hususan namna zinavyotumika katika shughuli za petroli ambazo zinategemea kwa kiasi kikubwa teknolojia, vifaa, huduma na mitaji kutoka nje ya nchi.

Aliiomba Serikali kuzingatia uwezekano wa kutoa misamaha au kuweka unafuu katika baadhi ya shughuli za petroli ili kuzingatia mahitaji maalumu ya kiutendaji ya sekta hiyo, huku maslahi ya Taifa yakiendelea kulindwa.

Alisema PURA itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu, kusimamia utekelezaji wa sheria na kanuni za petroli na kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi nchini zinasimamiwa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Naye Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga, aliipongeza menejimenti na watumishi wa PURA kwa kuboresha utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita ya Baraza la Wafanyakazi.

Alisema baraza hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mawasiliano kati ya menejimenti na wafanyakazi, kutatua changamoto za kikazi na kuboresha utendaji wa taasisi.

Luoga alitolea mfano azimio lililofikiwa katika mkutano wa tano wa baraza hilo uliofanyika Februari 2026, lililoitaka PURA kuandaa mkakati wa kufanya tafiti za awali kuhusu maeneo ya utafutaji wa mafuta na kubaini maeneo yanayoweza kuendelezwa zaidi.

Alisema hatua zimepigwa katika kuandaa mkakati huo pamoja na mipango ya utekelezaji wake, huku akiitaka Mamlaka hiyo kuendeleza kasi hiyo kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na kulinda maslahi ya Taifa.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad