HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 6, 2026

DODOMA YAIPONGEZA TASAC KWA KUUNGANISHA WADAU KUPUNGUZA FOLENI ZA MAGARI YA MIZIGO

  



Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Janeth Mayanja, ameipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa juhudi za kuwaunganisha wadau wa sekta ya uchukuzi katika kutafuta suluhisho la changamoto ya foleni za magari ya mizigo, pamoja na kuimarisha ufanisi wa usafirishaji wa shehena nchini.

Mayanja, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, ametoa pongezi hizo Novemba 5, 2026, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma wakati wa kikao na Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC iliyomtembelea ofisini kwake mkoani humo.

Amesema Dodoma ina fursa kubwa ya kuwa kitovu muhimu cha shughuli za usafirishaji na biashara nchini, hususan kupitia uwekezaji katika miundombinu ya bandari kavu, hatua itakayosaidia kupunguza msongamano wa magari ya mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kurahisisha usafirishaji wa shehena kwenda maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani.

Amesema mkoa huo una maeneo yenye fursa nyingi za uwekezaji, hivyo amewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuzitumia fursa hizo, akisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa iko tayari kushirikiana nao kuwezesha uwekezaji wenye tija kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Aidha, ameiomba TASAC kuwa balozi wa Mkoa wa Dodoma kwa kutangaza fursa zilizopo na kuhamasisha wawekezaji kuelekeza mitaji yao katika sekta ya uchukuzi, hususan ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya bandari kavu.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya bodi katika kufuatilia maendeleo ya miundombinu na shughuli za sekta ya uchukuzi, kutathmini hali halisi ya utoaji huduma na kuimarisha ushirikiano na Serikali za Mikoa pamoja na wadau mbalimbali.

Amesema katika ziara hiyo, bodi imetembelea maeneo ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) yaliyopo Ihumwa na Bahi mkoani Dodoma, yanayohusika na kuhudumia na kusafirisha shehena za mizigo kutoka ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa ziara hiyo inalenga kutathmini hali ya miundombinu na shughuli za usafirishaji katika maeneo hayo, kubaini fursa za uwekezaji na maeneo yanayohitaji maboresho, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati utakaosaidia kuongeza ufanisi wa huduma za usafirishaji na kupunguza changamoto zinazokwamisha mtiririko wa shehena nchini.
Juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa mizigo nchini kwa kuunganisha wadau, kuboresha miundombinu na kutumia fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad