HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 5, 2026

WADAU WAIPONGEZA TANZANIA KWA USIMAMIZI WA FEDHA ZA UMMA

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akieleza matokeo ya Programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma awamu ya sita (Public Finance Management Reform Programme - PFMRP VI) wakati wa Kikao cha Kamati ya Pamoja (Joint Steering Committee Meeting) kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kilichofanyika jijini Dar es Salaam.


Mwenyekiti Mwenza wa Wadau wa Maendeleo katika eneo la Usimamizi wa Fedha za Umma (Development Partners PFM Co-chair), Bw. Paul Welton (kulia), akizungumza wakati wa Kikao cha Kamati ya Pamoja (Joint Steering Committee Meeting) kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kuhusu utekelezaji wa Programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma awamu ya sita (Public Finance Management Reform Programme - PFMRP VI), kilichofanyika jijini Dar es Salaam. Katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, na kushoton ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Asha Khamis Abdullah.

Timu ya Wataalamu wa Serikali ya Tanzania (Kushoto) ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ikiwa katika Kikao cha Kamati ya Pamoja (Joint Steering Committee Meeting) kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo, ambacho kilijadili utekelezaji wa Programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma awamu ya sita (Public Finance Management Reform Programme - PFMRP VI), jijini Dar es Salaam.


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba (Katikati mstari wa mbele), Mwenyekiti Mwenza wa Wadau wa Maendeleo katika eneo la Usimamizi wa Fedha za Umma (Development Partners PFM Co-chair), Bw. Paul Welton (wa pili kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Asha Khamis Abdullah (wa pili kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Serikali na Wadau wa Maendeleo waliohudhuria Kikao cha Kamati ya Pamoja (Joint Steering Committee Meeting) kuhusu utekelezaji wa Programu ya maboresho ya usimamizi wa fedha za umma awamu ya sita (Public Finance Management Reform Programme - PFMRP VI), kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)


Na Joseph Mahumi na Peter Haule, WF, Dar es Salaam

Wadau wa Maendeleo wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma Awamu ya Sita (Public Finance Management Reform Programme - PFMRP VI), yaliyochangia kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za umma.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti Mwenza wa Wadau wa Maendeleo katika eneo la Usimamizi wa Fedha za Umma (Development Partners PFM Co-chair), Bw. Paul Welton, wakati wa kikao cha Kamati ya Pamoja (Joint Steering Committee Meeting) kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kuhusu utekelezaji wa Programu hiyox, kilichofunguliwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt Natu El-Maamry Mwamba, jijini Dar es Salaam.

Bw. Welton alisema kuwa mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango huo ni matokeo ya dhamira, uongozi wa kitaalamu na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali zinazotekeleza maboresho hayo pamoja na Wadau wa Maendeleo.

Alisema kuwa Benki ya Dunia imekamilisha tathmini ya katikati ya utekelezaji (Mid-Term Review) ya Programu ya Usimamizi wa Fedha za Umma na Mifumo ya Ununuzi kwa Utoaji Huduma, na tathmini hiyo imebaini mafanikio muhimu katika maeneo ya uhamasishaji na ukusanyaji wa mapato ya ndani, ufanisi wa mifumo ya ununuzi wa umma, usimamizi wa uwekezaji wa umma, uwazi wa bajeti pamoja na ukaguzi wa nje na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.


“Mafanikio hayo yamechangia kuboresha matokeo ya matumizi ya rasilimali za umma kwa wananchi, kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma na kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa rasilimali zinazoweza kusaidia maendeleo na upanuzi wa ajira nchini” alisema Bw. Welton

Alisisitiza kuwa maboresho ya usimamizi wa fedha za umma yana umuhimu mkubwa katika kufanikisha Dira 2050, hususan katika kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa ufanisi na kuelekezwa katika shughuli zinazochochea maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendeleza na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma nchini kwa kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma Awamu ya Sita yanadumishwa na kujengwa zaidi katika awamu ya saba ya mpango huo.

Alisema kuwa Mpango huo umeleta mafanikio makubwa na matokeo yanayoonekana katika kuimarisha usimamizi wa mapato na matumizi ya Serikali, uwajibikaji, ufanisi na uwazi katika mifumo ya fedha za umma, ikiwemo kuanzishwa kwa Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NEST), ambao umechangia kupunguza muda wa michakato ya ununuzi na kuongeza thamani ya fedha katika manunuzi ya umma.


“Miongoni mwa mafanikio ni kuongezeka kwa idadi ya walipakodi kutoka milioni 1.6 mwaka 2023 hadi milioni 2.5 kufikia Juni 2026, hatua iliyoiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi na kuongeza ufanisi katika kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato, ikiwemo kupitia kampeni za nyumba kwa nyumba” alisema Dkt. Mwamba.

Aliongeza kuwa, Mafanikio mengine ni pamoja na kuandaliwa na kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya mwaka 2025, ujenzi wa jengo la Wizara ya Fedha mkoani Geita kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma, pamoja na kuandaliwa na kuingizwa kwa mifumo ya ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi katika mfumo wa TAUSI unaotumiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Dkt. Mwamba alitaja pia kuanzishwa kwa Mfumo wa Malipo ya Wastaafu wa Hazina (Treasury Pensioners Payment System), unaolenga kuboresha utambuzi na malipo ya wastaafu, Mfumo wa Malipo wa Pamoja (Universal Billing System) unaowezesha utoaji wa bili kwa utaratibu mmoja, pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Magari ya Serikali (Fleet Management System) unaolenga kudhibiti matumizi ya magari na kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma.

Aliwashukuru na kuwahimiza Wadau wa Maendeleo kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa awamu inayofuata ya mpango huo ili kuimarisha zaidi uwazi, uwajibikaji, ufanisi na tija katika usimamizi wa fedha za umma kwa manufaa ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad