HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 29, 2026

MALAIKA GRAY, MARIOO WAUNGANISHA VIPAJI KWENYE ‘MY FEVER’

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MWIMBAJI na mtunzi wa nyimbo Mtanzania, Malaika Gray, ameanza safari yake rasmi ya muziki kwa kutoa wimbo wake wa kwanza, My Fever, akimshirikisha nyota wa Bongo Flava, Marioo.

Wimbo huo uliotoka Oktoba 30, 2026, umeandaliwa jijini Dar es Salaam, ambako pia video yake ilirekodiwa katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, ukiwemo ufukwe wa Bahari ya Hindi, masoko, vituo vya daladala na mitaa ya kawaida.

Malaika amesema ameamua kuanzia nyumbani kwa sababu Tanzania ndiyo sehemu yenye nafasi ya pekee katika maisha na safari yake ya muziki, ingawa dhamira yake ni kutengeneza nyimbo zitakazowafikia wasikilizaji duniani kote.

“Niliutengeneza nyumbani kwa sababu ndiko moyo wangu ulipo, Tanzania na bara ninalolijua na kulipenda. Lakini ninatengeneza muziki kwa ajili ya yeyote atakayeusikia. Nyumbani ndipo unapoanzia, si pale unapoishia,” amesema.
My Fever ni wimbo wa mapenzi unaoelezea mvuto na hisia zinazojengeka kati ya watu wawili, ukiunganisha midundo ya Afrobeats na Bongo Flava pamoja na ladha ya R&B, inayochangiwa na uzoefu wa Malaika kukulia katika nchi mbalimbali.

Msanii huyo amesema aliandika wimbo huo akilenga kuwasilisha hisia za mapenzi zinazochanganyika na mazingira ya kiangazi, huku akitaka sauti na ladha yake viakisi maisha ya Dar es Salaam.

Malaika aliandika wimbo huo kwa kushirikiana na Marioo, huku Abbah Process akihusika katika utayarishaji wa muziki huo.

Video ya My Fever ilirekodiwa kwa siku mbili jijini Dar es Salaam chini ya uongozi wa Joma, ikionesha mandhari na maisha ya kila siku ya jiji hilo. Marioo pia anaonekana katika video hiyo, iliyotolewa kupitia chaneli za wasanii hao wawili.
Kwa upande wake, Marioo amesema amefurahishwa na ushirikiano huo, akieleza kuwa Malaika ana kipaji na anaamini wataendelea kufanya kazi pamoja katika siku zijazo.

“Malaika ana kipaji cha kweli, na ilikuwa furaha kwangu kushiriki katika wimbo wake wa kwanza. Natarajia tutafanya kazi nyingi zaidi pamoja,” amesema Marioo.

Malaika, aliyekulia kati ya Tanzania na Afrika Kusini, kwa sasa anasomea Vocal Performance na Music Business katika Chuo cha Muziki cha Berklee kilichopo Boston, Marekani.

Kutolewa kwa My Fever ni mwanzo wa safari yake ya muziki, huku kukiwa na mipango ya kutoa kazi nyingine na kufanya ushirikiano wa kimuziki katika Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika hadi mwaka 2027.

Wimbo huo umetolewa kupitia Africori, kampuni inayohusishwa na Warner Music Group, na unapatikana katika majukwaa mbalimbali ya kidijitali ya kusikiliza muziki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad