Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Kanda ya Mashariki, imebaini kuwa maduka 19 kati ya 38 ya dawa muhimu yaliyokaguliwa katika Wilaya ya Mafia hayakuwa na watoa huduma wenye sifa zinazotakiwa kisheria, sawa na asilimia 50 ya maduka yote yaliyokaguliwa.Hali hiyo imeibua wasiwasi kuhusu usalama wa wananchi wanaopata huduma za dawa kutoka kwa watu wasio na sifa zinazotakiwa kisheria.
Matokeo hayo yamebainika katika ukaguzi maalumu uliofanywa na TMDA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia kuanzia Oktoba 11 hadi 23, 2026.
Ukaguzi huo ulilenga kuhakikisha kuwa maduka ya dawa na maeneo yanayotoa huduma zinazohusiana na dawa na vifaa tiba yanaendesha shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo husika.
Akitoa mrejesho wa ukaguzi huo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mkaguzi Mwandamizi wa Dawa aliyeongoza timu hiyo, Japhari Saidi, alisema kuwa mbali na ukosefu wa watoa huduma wenye sifa, ukaguzi ulibaini ukiukwaji mwingine wa sheria na taratibu zinazosimamia uendeshaji wa maduka ya dawa muhimu.
Alisema maduka 10 yalibainika kufanya biashara bila vibali vinavyotakiwa, kinyume na Kifungu cha 18 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, sawa na asilimia 26.3 ya maduka yaliyokaguliwa.
Aidha, maduka 13 yalikutwa yakiuza dawa ambazo haziruhusiwi kuuzwa katika maduka ya dawa muhimu, sawa na asilimia 34.2. Maduka mengine sita yalibainika kuuza dawa zisizosajiliwa, kinyume na Kifungu cha 22 cha sheria hiyo, sawa na asilimia 15.8.
Katika ukiukwaji mwingine, maduka matatu yalikutwa yakitoa huduma za kitabibu, ikiwemo vipimo vya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), kinyume na matakwa ya sheria.
Kufuatia matokeo hayo, TMDA ilichukua hatua za kiudhibiti kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kuondoa dawa ambazo hazikustahili kuuzwa katika maduka hayo na kuyaelekeza maduka yasiyokuwa na watoa huduma wenye sifa kusitisha huduma hadi yatakapokidhi matakwa ya kisheria.
Vilevile, faini za papo kwa papo zilitolewa kwa makosa yaliyostahili hatua hiyo, ambapo jumla ya Sh milioni 2.9 zilitozwa. Kufikia Oktoba 25, 2026, faini zote zilikuwa zimelipwa.
Kwa upande wake, Mfamasia wa Wilaya ya Mafia, Kurwa Lucas, aliipongeza TMDA kwa ushirikiano wake na halmashauri hiyo, akiahidi kuendelea kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa kwa wamiliki wa maduka husika.
Alisema ufuatiliaji huo utasaidia kuhakikisha maduka yanafuata matakwa ya kisheria na kutoa huduma zinazokidhi viwango vinavyotakiwa.
Hatua hizo zinalenga kulinda afya za wananchi wa Mafia dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na dawa zisizosajiliwa, uuzaji wa dawa zisizoruhusiwa na utoaji wa huduma na watu wasio na sifa zinazotakiwa kisheria.

No comments:
Post a Comment