HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, October 3, 2026

CHONGOLO AITAKA ASA KUZALISHA MBEGU KWA TIJA



WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amewataka watumishi wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kufanya kazi yenye tija inayoonekana, maarifa na ubunifu ili kuleta matokeo kwa wananchi.

Amesema akiwa katika ziara ya kikazi kukagua shughuli za uzalishaji wa mbegu katika Shamba la Mbegu la Kilimi linalosimamiwa na Wakala wa Mbegu za Kilimi (ASA) tarehe 2 Oktoba 2026, mkoani Tabora.

“Niwaombe tujielekeze kwenye matokeo, tutafute matokeo kwa kutengeneza jambo kwa tija. Kila mmoja ataliona na watu watasema jambo hili limefanyika,” amesema, akisisitiza kuwa mafanikio ya uzalishaji wa tani mbalimbali katika shamba hilo si jambo dogo bali ni matokeo ya kazi iliyofanyika.

Shamba la Mbegu la Kilimi ni miongoni mwa mashamba yanayomilikiwa na ASA yenye jukumu la kuweka msukumo wa uzalishaji wa mbegu nchini ili kupunguza utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi.

Aidha, Mhe. Chongolo ameielekeza ASA kuongeza uwekezaji wa miundombinu ya umwagiliaji, ili kuhakikisha msimu ujao uzalishaji unaongezeka kwa kiwango kikubwa zaidi.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa ASA, Mhandisi Innocent Masaka, amesema shughuli za uzalishaji katika Shamba la Mbegu la Kilimi kwa sasa zinafanyika kwa misimu miwili kwa mwaka kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika miundombinu ya umwagiliaji, ambapo eneo lenye ukubwa wa ekari 1,000 limewekewa miundombinu hiyo.

Amesema katika msimu wa masika, shamba lilizalisha mbegu za Mahindi katika hekta 142 na Alizeti katika hekta 119, ambapo tani 231.900 za Mahindi na tani 40.300 za Alizeti tayari zimesafirishwa kwenda Makao Makuu ya ASA Morogoro kwa ajili ya uchakataji, huku kilo 8,800 za mbegu za Alizeti zikiwa bado shambani zikisubiri kusafirishwa.

Kwa msimu wa kiangazi, shamba limezalisha mbegu za Maharage aina ya Uyole Njano katika eneo la hekta 40, ambapo zao hilo liko katika hatua ya kukomaa na linatarajiwa kutoa tani 40 za mbegu.

Mhandisi Masaka amesema kwa msimu wa kilimo wa 2026/2027, Shamba la Kilimi linatarajia kupanda hekta 145 za Mahindi na hekta 155 za Alizeti, kwa matarajio ya kuvuna tani 363 za Mahindi na tani 155 za Alizeti.









No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad