HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 4, 2026

MWANAFUNZI WA TIA ABUNI TEKNOLOJIA YA KUPUNGUZA UDANGANYIFU KATIKA UNUNUZI WA PAMBA

Na Mwandishi Wetu
MWANAFUNZI wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Paschal Sabuni Shija, amebuni mfumo wa kidijitali unaounganishwa na mizani ya kupimia pamba kwa lengo la kumwezesha mkulima kupata taarifa sahihi za uzito wa pamba yake na kurahisisha ufuatiliaji wa malipo.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya NaneNane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, jijini Dodoma, Shija amesema ubunifu wa mawazo ya Kiteknolojia utasaidia jamii kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuibua fursa za ajira.

"Nimekuwa miongoni mwa wanafunzi wanaonufaika na mpango wa TIA wa kukuza, kuendeleza vipaji na taaluma jambo linalonisaidia kuendeleza wazo ili kutatua changamoto kwa jamii",amesema Shija.

" TIA imekuwa ikinisimamia kunipa mwongozo katika kuboresha ubunifu huu ili kutoa suluhisho la changamoto zinazowakabili wakulima wa pamba na mazao mengine",amesema Shija.

Mfumo huu utamsaidia mkulima anapopima pamba kupata taarifa ya uzito wa mazao hayo moja kwa moja kwenye simu yake ya mkononi, sambamba na kupatiwa stakabadhi yenye taarifa za muamala.

Shija alisema mfumo huo pia utasaidia kuongeza uwazi katika mchakato wa ununuzi wa pamba na kupunguza mianya ya udanganyifu ambayo imekuwa ikiwakatisha tamaa baadhi ya wakulima kuendelea na kilimo cha zao hilo.

Matumizi ya teknolojia katika sekta ya kilimo ni muhimu kwa kuwa yanamwezesha mkulima kupata taarifa kwa wakati, kufuatilia mazao yake na kuwa na ushahidi wa miamala inayohusiana na mauzo,Aliongeza Shija.

Aidha, Shija alisema mpango wa TIA wa kuendeleza mawazo na ubunifu wa wanafunzi una nafasi kubwa katika kuongeza fursa za ajira, hususani kwa vijana wanaohitimu masomo ya vyuo mbalimbali,kwani inaweza kuwa chanzo cha kujiajiri na suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.

Alisema ubunifu unaotokana na wanafunzi unaweza kuwa chanzo cha kujiajiri na pia kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali zinazolikabili Taifa.

"Ninatoa wito kwa vijana kutumia maarifa wanayopata vyuoni kubuni teknolojia zitakazokuwa na manufaa kwa jamii", amesema Shija.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad