HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 20, 2026

MNMA YAJIVUNIA UBUNIFU WA VIJANA KATIKA KUWAFUNGULIA FURSA MBALIMBALI

 




Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) Profesa Haruni Mapesa, amesema maonyesho ya elimu, ujuzi na ubunifu ni jukwaa muhimu kwa taasisi za elimu kuonyesha kazi zinazofanywa na wanafunzi pamoja na kuwafungulia vijana fursa mbalimbali za kujifunza na kuendeleza vipaji vyao.

Profesa Mapesa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kuhusu ushiriki wa chuo hicho katika maonyesho ya elimu, ujuzi na ubunifu yanayoendelea mkoani Tanga, akimpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, pamoja na Wizara hiyo kwa kuendelea kusimamia maonyesho hayo na kuwa na mafanikio.

Amesema maonyesho hayo yamekuwa na umuhimu kwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuwa yanatoa nafasi ya kuonyesha programu zinazotolewa na chuoni ikiwemo mafunzo yanayohusiana na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), pamoja na kazi za ubunifu zinazofanywa na wanafunzi.

“Tunajivunia kupata fursa ya kuonyesha kazi za vijana wetu, ubunifu wao katika sayansi, teknolojia na maeneo mbalimbali. Ubunifu huu umekuwa na mguso mkubwa na tunaamini siku zijazo utakuwa na matokeo makubwa zaidi,” amesema Profesa Mapesa.

Amesema chuo kina mpango wa kuendeleza ubunifu wa wanafunzi kwa kuunganisha kazi hizo na watumiaji na wadau wakubwa ili zitumike zaidi katika shughuli za uzalishaji na kuchangia maendeleo ya uchumi.

Profesa Mapesa amesema maonyesho hayo pia yamekuwa fursa kwa vijana wanaotaka kujiunga na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kupata taarifa kuhusu programu mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho, huku baadhi yao wakipata huduma za usajili na maelekezo ya kujiunga na programu hizo moja kwa moja katika banda la chuo.

Ameeleza kuwa chuo kinatoa programu za umahiri, shahada ya kwanza, pamoja na diploma, huku akiwataka wananchi wa Tanga kutembelea maonyesho hayo, hususan banda la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ili kupata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu huduma na programu zinazotolewa na taasisi hiyo.

Aidha, amesema chuo hicho kina nafasi ya kipekee katika kuhifadhi na kutangaza historia ya Muasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia machapisho, kumbukumbu na hotuba zake ambazo, amesema, zimekuwa na mchango mkubwa katika historia ya Tanzania na Afrika.

Profesa Mapesa amewashukuru waandaaji wa maonyesho hayo pamoja na vyombo vya habari kwa kuendelea kuhabarisha umma kuhusu shughuli za maonyesho na kazi zinazofanywa na taasisi za elimu. Pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusisitiza umuhimu wa elimu, ujuzi na ubunifu katika maendeleo ya taifa.

Amesema uwekezaji unaoendelea katika elimu, ujuzi na ubunifu ni muhimu katika kujenga Taifa lenye vijana wenye uwezo wa kutumia maarifa na teknolojia kutatua changamoto na kuchangia maendeleo ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad