Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewataka Waandishi wa Habari wa Crown Media kulinda imani ya umma kwa kuzingatia weledi, maadili, uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo ya siku mbili yaliyotolewa na JAB kwa Waandishi wa Habari wa Crown Media, kuanzia Agosti 18 hadi 19, 2026, jijini Dar es Salaam yakilenga kuwaongezea maarifa na kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, maadili na viwango vya taaluma ya uandishi wa habari.
Akiwasilisha Mada kuhusu Msingi na Mfumo wa Kisheria unaosimamia Sekta ya Habari nchini Tanzania katika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amewasihi Waandishi wa Habari kuthamini na kulinda taaluma yao kwa kuzingatia misingi inayowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wake, Dkt. Egbert Mkoko amewataka Waandishi wa Habari kuzingatia maadili katika kila hatua ya kazi zao, akieleza kuwa maadili ndiyo msingi wa uandishi wa habari unaowajibika na wenye tija kwa jamii.
“Mwandishi wa Habari anapaswa kuzingatia maadili ya kazi katika kila hatua ya utekelezaji wa majukumu yake, kwa kuwa uadilifu na uwajibikaji ndiyo msingi wa taaluma hii,” amesema Dkt. Mkoko alipokuwa akifafanua mada Kuhusu Maadili ya Utangazaji na makosa ya kimaadili yanayofanywa mara kwa mara.
Naye Mjumbe wa JAB na Kaimu Meneja wa Huduma za Kiswahili wa Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN), Bw. Mgaya Kingoba, akiwasilisha mada kuhusu uzalendo, amewataka Waandishi wa Habari kutumia taarifa kwa usahihi na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya umma.

“Kwa kweli, changamoto tuliyonayo katika vyombo vyetu vya habari ni kushindwa kutofautisha maoni binafsi na uchambuzi wa kitaaluma, pamoja na kushindwa kutenganisha nafasi ya mtu binafsi na wajibu wake kama mwanataaluma. Pia kumekuwa na dhana kwamba Bodi ipo kwa ajili ya kuwadhibiti Waandishi wa Habari, pamoja na uelewa mdogo kuhusu ithibati, umuhimu wake na nafasi yake katika kulinda heshima ya taaluma,” amesema Imani Luvanga mmoja wa washiriki.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya JAB kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, yanayolenga kuimarisha weledi, uadilifu, uwajibikaji na tija katika taaluma ya uandishi wa habari.











No comments:
Post a Comment