HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, August 30, 2026

DC CHATO: HUDUMA ZA OSHA NI MUHIMU KWA UKUAJI ENDELEVU WA UCHUMI

 

Mkuu  wa Wilaya ya Chato, Mhe. Louis Peter Bura, akikabidhi vifaa kinga vilivyogharamiwa na Serikali kwa mafundi wa uchomeleaji vyuma na useremala katika Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe Wilaya ya Chato. Mafundi hao walipatiwa mafunzo ya usalama na afya kazini na OSHA na kisha kukabidhiwa vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na kofia ngumu, glovu, barakoa na makoti ya usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Mhe. Louis Peter Bura akifungua mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa kikundi cha mafundi wanaojihusisha na uchomeleaji vyuma na useremala katika Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.
Mwanakikundi cha Smart Welders and Funirtures, kilichopo Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe, Wilaya Chato, akionesha mfano wa matumizi sahihi ya vifaa kinga katika shughuli za uchomeleaji vyuma baada ya kushiriki mafunzo ya usalama na afya kazini yaliyotolewa na Taasisi ya OSHA kwa wanakikundi tajwa.
Meneja wa OSHA Kanda ya Ziwa, Lodgard Bishanga, akiwasilisha mada katika mafunzo ya kuwajengea uelewa wa vihatarishi vya kiusalama na afya mafundi wa uchomeleaji vyuma na useremala katika Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe Wilaya ya Chato.

Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Chato, Mhe. Louis Peter Bura, amesema kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi katika Mkoa wa Geita imepelekea uhitaji wa huduma za usalama na afya mahali pa kazi kuongezeka ambapo ameutaka Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuhakikisha upatikanaji wa huduma za ukaguzi na ushauri wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.

Ametoa kauli hiyo wakati akifungua mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA kwa kikundi cha mafundi wanaojihusisha na uchomeleaji vyuma na useremala katika Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.

Mafunzo hayo ambayo ni sehemu ya utekelezaji mpango mkakati wa Taasisi ya OSHA yametolewa kwa watu 15 ambao ni wanakikundi cha Smart Welders and Funirtures ambao kituo chao kimekuwa kikitumika kutoa mafunzo ya ufundi kwa wananchi wa Kata ya Nyamirembe na maeneo ya karibu.

Mkuu wa Wilaya huyo amesema kwa kipindi cha miaka mitatu tangu mwaka 2024, Wilaya ya Chato imeshuhudia ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi zikiwemo shughuli za uchimbaji madini.

“Kipekee niwashukuru sana OSHA kwa kuendelea kutekeleza ipasavyo jukumu lenu la msingi la kusimamia usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini. Lakini naomba niwakumbushe kwamba maeneo mengi yanayokuwa kiuchumi yanahitaji sana huduma zenu ambapo Mkoa wa Geita hususan Wilaya ya Chato ni miongoni mwa maeneo hayo,” ameeleza Mheshimiwa Bura na kuongeza:“Hivyo, niwaombe kuangalia maeneo haya kwa jicho la pekee kwani huko nyuma mlikuwa hamjulikani lakini kwasasa watu wanawatambua umuhimu wenu na wanahitaji huduma zenu za ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya, uchunguzi wa afya za wafanyakazi, mafunzo na ushauri wa kitaalam juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi.”

Aidha, DC Bura amewapongeza OSHA kwakutoa mafunzo na msaada wa vifaa kinga kwa kikundi cha mafundi ambao shughuli zao zinagusa maisha ya maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Chato.

Ameahidi kuendelea kushirikiana na OSHA katika kuhamasisha wakazi wa Chato kuzingatia kanuni bora.

Meneja wa OSHA Kanda ya Ziwa, Lodgard Bishanga, amesema mafunzo husika usalama na afya katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazotekelezwa katika Wilaya hiyo huku akiwataka wamiliki wa maeneo ya kazi kuwapa ushirikiano wataalam wa OSHA.

Amesema lengo la kuwajengea uelewa wa vihatarishi vya kiusalama na afya katika shughuli zao za ufundi pamoja na mbinu za kudhibiti vihatarishi husika.

“Sambamba na kupatiwa mafunzo, washiriki wamekabidhiwa vifaa kinga vya mfano yakiwemo makoti ya usalama, glovu, kofia ngumu na barakoa ambavyo vimegharamiwa na serikali kama sehemu ya kuendelea kuhamasisha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika shughuli za uzalishaji

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo Lulinda Makoye Manyema naNeema Kalebo wameishukuru Serikali kwakuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya kazini pamoja na kuwapatia vifaa kinga.

“Tumejifunza mambo mengi sana kupitia mafunzo haya ikiwemo jinsi ya kukuza na kulinda usalama tunapokuwa katika karakana zetu ikiwemo kuwa na mpangilio mzuri wa mashine na vifaa.

Aidha, tumejifunza jinsi ya kutoa huduma ya kwanza endapo itatokea ajali katika shughuli zetu za kila siku,” ameeleza Neema Kalebo, mshiriki wa mafunzo.

Wanakikundi cha Smart Welders and Funirtures, kilichopo Kijiji cha Kalebezo, Kata ya Nyamirembe, Wilaya Chato, wakiwa katika picha ya pamoja na Meneja wa Kanda ya Ziwa wa OSHA, Lodgard Bishanga (wakwanza kushoto) na Afisa Maendeleo Nyamirembe, Sarah Seizure Hamza (wakwanza kulia) baada ya kushiriki mafunzo ya usalama na afya kazini yaliyotolewa na Taasisi ya OSHA kwa wanakikundi tajwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad