HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 2, 2026

Mkenda: Sayansi na Ubunifu Viwe Chachu ya Uchumi wa Taifa

 


Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ameitaka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kujitathmini kwa uhalisia wanapokwenda kuadhimisha miaka 40 badala ya kujikita zaidi katika kusherehekea mafanikio.

Profesa Mkenda ametoa wito wa tafakuri hiyo leo Julai 2, 2026 jijini Dar es salaam wakati wa uzunduzi wa miaka 40 ya COSTECH (COSTECH@40) pamoja na Mfumo wa Taifa wa Taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (National Information System for Science, Technology and Innovation – NISSTI).

Akizungumza wakati wa uzunduzi huo, amesema tathmini ya miaka 40 ya Costech inapaswa kuwa ya kina na yenye kuangalia mchango halisi wa sayansi katika maisha ya watanzania, akisisitiza sayansi na ubunifu vinapaswa kupimwa kwa matokeo yaliyo wazi na sip kwa sherehe au taswira za nje.

Utafiti unahitaji uhuru wa kitaaluma, lakini mafanikio yake yanategemea uratibu madhubuti, ushirikiano wa sekta zote na mfumo wa kitaifa unaounganisha juhudi za taasisi mbalimbali kwa maendeleo ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu." Amesems Prof. Mkenda

"Sera yetu mpya lazima iendane na mahitaji ya wakati na iwe chachu ya mageuzi. Tuwe na ndoto kubwa, tufikiri picha pana na tuthubutu kuchukua hatua, kwa sababu bahati huwapendelea wanaothubutu.

Aidha ametoa wito kwa watafiti, taasisi za utafiti, wavumbuzi na wadau wote kujisajili kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (NISSTI) na kuhakikisha taarifa zao zinahuishwa mara kwa mara na kwamba Mafanikio ya mfumo huo yanategemea ushiriki wa kila mmoja."

"Nawaalika vijana wa Tanzania kuikumbatia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kama njia ya kutatua changamoto za jamii, kuunda ajira na kuijenga Tanzania yenye uchumi shindani unaotegemea maarifa, ubunifu na teknolojia. Mustakabali wa Taifa letu uko mikononi mwa vijana wake."

Amesisitiza sayansi na teknolojia lazima zielekezwe kuongeza tija na mavuno kwa wakulima ili Tanzania iweze kushindana katika masoko ya kimataifa na kuinua uchumi wa wananchi wake, hivyo matokeo ya utafiti yanapaswa kuonekana sokoni na si kaulimbiu au maonesho ya muda.

Pia alisisitiza taasisi za utafiti kuchunguza kisayansi tiba za asili kwa kufanya majaribio ya awali na ya kitabibu ili kuthibitisha uhalisia wake ili kama zinafanya kazi zigeuzwe kuwa bidhaa rasmi za dawa na kama hazifanyi kazi basi wananchi waelezwe.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Caroline Nombo alisema wanapoadhimisha miaka 40 wanapata nafasi ya kutafakari historia ya uwekezaji wa Serikali katika sayansi, teknolojia na ubunifu pamoja na mchango wake katika kutatua changamoto za jamii.

"Kipaumbele chetu ni kuhakikisha maarifa yanayozalishwa katika vyuo vikuu, taasisi za utafiti, maabara, vituo vya ubunifu na sekta binafsi yanachangia maendeleo ya sekta za kipaumbele za taifa." Amesema.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa NISST Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dkt. Amos Nungu amesema maadhimisho ya COSTECH@40 si ya kuangalia tulikotoka pekee, bali ni ya kujenga Tanzania tunayoitaka kupitia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kuelekea Dira ya Taifa 2050."

"Sayansi na ubunifu lazima vionekane, vieleweke, vifikike kwa urahisi na viwe na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi." Amesema Prof. Nungu.

Amesema, mustakabali wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini utajengwa kwa ushirikiano, maarifa ya pamoja na ushiriki wa wadau wote hivyo tunataka kila mtafiti, mbunifu na taasisi ionekane, iunganishwe na ipate fursa kupitia mfumo mmoja wa kitaifa."

"Miaka 40 ya COSTECH ni urithi wa mafanikio; miaka 40 ijayo lazima iwe safari ya matokeo makubwa zaidi kwa maendeleo ya taifa.... Ushindani wa Tanzania katika uchumi wa maarifa utaimarishwa kwa kuwekeza katika Sayansi, Teknolojia na Ubunifu." amesema Dkt Nungu.

Naye John Kondoro, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Costech amesema, Costech taendelea kuisimamia Tume kwa karibu ili kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kwa weledi, kwa wakati na kwa matokeo yanayopimika."

"Taarifa zinazopatikana kupitia NISSTI zinapaswa kuwa msingi wa kupanga vipaumbele vya taifa, kuelekeza uwekezaji na kuongeza tija ya utafiti na ubunifu".


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad