HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 2, 2026

Hakuna Bunge Dhaifu, Lote Lina Jukumu la Kusimamia Ustawi wa Wananchi – Zungu

 

SPIKA wa Bunge, Mussa Zungu, amesema hakuna Bunge gumu, kali, bovu wala dhaifu, akisisitiza kuwa jukumu la Bunge ni moja tu, kuhakikisha ustawi wa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Zungu alieleza hayo akijibu maswali ya baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari katika mkutano wake na wahariri hao kuhusu maadhimisho ya miaka 100 ya Chimbuko la Bunge uliofanyika jana Dar es Salaam. Akijibu swali kuhusu mtazamo kuwa Bunge la sasa ni dhaifu kutokana na uwepo wa idadi ndogo ya wabunge wa upinzani, alisema mtazamo huo si wa kweli.

Alisema hakuna Bunge lililokuwa bovu, kali au dhaifu, kwani mabunge yote yana jukumu moja la kusimamia ustawi wa jamii kupitia sekta mbalimbali ikiwemo mazingira, afya, elimu na makazi ya wananchi.

“Naomba niseme kitu tena hili mchukue maelezo, hakuna Bunge dhaifu, hatupigani, Bunge siyo klabu ya mapambano, bungeni tunakaa, tunajenga hoja na tunajibu hoja kwa hoja,” alisema.

Alisema si sahihi kulitaja Bunge kuwa dhaifu kwa sababu halijaitaka Serikali kuondoa kodi ya bodaboda au kodi ya kilimo, akieleza kuwa Bunge limekuwa likitoa maelekezo kwa Serikali kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo sera za kodi na matumizi ya magari ya gharama kubwa.

Aliongeza kuwa mawaziri husimama Bungeni kueleza msimamo wa Serikali, lakini pale ambapo Bunge halikubaliani na Serikali, hutoa maelekezo kwa kuwa ni mhimili wa dola wenye jukumu la kuisimamia Serikali.

Kuhusu hoja ya Bunge kukosa mvuto kutokana na idadi ndogo ya wabunge wa upinzani, Zungu alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 vyama vya upinzani vilipata jumla ya wabunge 102 chini ya Katiba na Tume ileile ya Uchaguzi, na kambi rasmi ya upinzani iliundwa baada ya kufikia idadi iliyohitajika.

“Mtakumbuka mwaka 2015 upinzani ulikuwa na nguvu kubwa ndani ya Bunge. Dar es Salaam kulikuwa na majimbo mengi ya upinzani ikiwemo Kinondoni, Ubungo na Kigamboni. Hata katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa walishinda maeneo mengi,” alisema.

Alisema wananchi waliwapa nafasi ya kuongoza katika maeneo mbalimbali, lakini hali ya sasa ya kuwa na wabunge wachache wa upinzani ni matokeo ya maamuzi ya wananchi kupitia uchaguzi. “Kwa uongozi wa vyama vya siasa wa sasa wanaviongozi wazuri lakini bado hawajawa na hamasa ya kuwashawishi wananchi vya kutisha ili kuwachagua,” alisema Zungu.

Awali, akizungumzia maadhimisho ya miaka 100 ya Chimbuko la Bunge, Zungu alisema Bunge limepitia mabadiliko mbalimbali ya kanuni yaliyosaidia kuimarisha demokrasia, maendeleo ya taifa na ushiriki wa wananchi katika uongozi. Alisema ushiriki wa wanawake umefikia asilimia 40, huku idadi ya wabunge vijana ikifikia 72 na wabunge wenye ulemavu kufikia 11, hatua aliyoeleza kuwa inaonesha mafanikio ya maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 100 ya Bunge.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad