HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, July 12, 2026

HIFADHI SKIMU NI MKOMBOZI KWA WANANCHI WALIOJIAJIRI”– MHE. KAFITI

  Dar es Salaam, Julai 12, 2026


Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mhe. William Kafiti, amesema Hifadhi Skimu ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) imeendelea kuwa mkombozi kwa wananchi waliojiajiri kwa kuwapa fursa ya kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha ya baadaye, huku akiipongeza NSSF kwa kuimarisha huduma kwa wanachama kupitia mifumo ya kidijitali na utoaji wa huduma wenye viwango vya juu.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la NSSF katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mhe. Kafiti alisema ameridhishwa na kiwango cha huduma kinachotolewa na Mfuko huo, akibainisha kuwa wananchi wanapokelewa na kuhudumiwa kwa weledi, haraka na kwa kutumia teknolojia ya kisasa inayorahisisha upatikanaji wa huduma.

"Nimefurahishwa sana na huduma nilizoziona hapa, kila mfanyakazi yuko tayari na ana ari ya kumhudumia mwananchi kwa weledi na kwa wakati. Hili linaonesha dhamira ya kweli ya NSSF ya kuwahudumia Watanzania kwa viwango vya hali ya juu," alisema Mhe. Kafiti.

Alisema mafanikio hayo yanaakisi jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuimarisha sekta ya hifadhi ya jamii na kupanua wigo wa huduma kwa wananchi wote, hususan waliojiajiri ambao kwa miaka mingi walikuwa nje ya mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii.

Mhe. Kafiti alieleza kuwa kuanzishwa kwa Hifadhi Skimu kumefungua ukurasa mpya kwa makundi mbalimbali ya wananchi waliojiajiri, wakiwemo bodaboda, mama na baba lishe, wafanyabiashara wadogo, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, mafundi na makundi mengine ya wajasiriamali, kwa kuwawezesha kujiwekea akiba itakayowawezesha kuwa na uhakika wa kipato wanapofikia uzee.

"Kila mmoja atazeeka. Kesho iliyo bora hujengwa na maamuzi ya leo. Kupitia Hifadhi Skimu, NSSF imewapa wananchi waliojiajiri fursa ya kujenga maisha yenye uhakika baada ya kipindi chao cha kufanya kazi. Huu ni mpango unaostahili kuungwa mkono na kila Mtanzania," alisisitiza.

Aidha, aliipongeza NSSF kwa maboresho makubwa ya mifumo ya kidijitali yanayowawezesha wanachama kupata taarifa za michango yao kwa urahisi kupitia simu za mkononi, hatua aliyoielezea kuwa ni mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za hifadhi ya jamii.

Mhe. Kafiti aliongeza kuwa NSSF inaendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya kujenga taifa lenye wananchi wanaojitegemea kiuchumi kwa kuwawezesha kuweka akiba wakiwa bado wana nguvu za kufanya kazi ili wanapostaafu waendelee kuishi kwa heshima kupitia mafao na pensheni wanazostahili.

Naye, Theonasy Ngunga, mmoja wa wananchi waliotembelea banda la NSSF alieleza kuridhishwa na huduma alizopata, akisema alipokelewa kwa heshima, akaelekezwa katika kila hatua na ndani ya muda mfupi akapatiwa elimu kuhusu Hifadhi Skimu na kukamilisha taratibu za kujiunga na NSSF Portal.

"Nilipoingia nilipokelewa vizuri na kupewa maelekezo katika kila hatua. Ndani ya muda mfupi nilikuwa nimehudumiwa na kuelewa namna ya kuchangia kupitia mifumo popote nilipo," alisema.

Kupitia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, NSSF inaendelea kuwahamasisha wananchi, hususan waliojiajiri, kujiunga na Hifadhi Skimu ili kujenga akiba kwa ajili ya maisha ya baadaye. Juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya hifadhi ya jamii na kujenga kesho yenye uhakika kupitia mfumo endelevu wa hifadhi ya jamii.













No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad