
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Wasafi Media, Nasib Abdul maarufu Diamond Platnumz, amesema utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari unaweka mazingira bora ya kukuza uwekezaji katika sekta ya habari kwa kuhakikisha vyombo vya habari vinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, weledi na viwango vya taaluma.
Diamond alitoa kauli hiyo tarehe 11 Juni, 2026 alipotembelea Banda la Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), kufuatia mwaliko wa Bodi hiyo ili kujionea huduma na elimu inayotolewa kwa waandishi wa habari pamoja na wananchi.
Alisema uwekezaji katika sekta ya habari unahitaji nidhamu, maono, subira na uongozi unaozingatia sheria, akibainisha kuwa usimamizi unaofanywa na JAB unasaidia wawekezaji kuelewa matakwa ya kisheria na namna ya kuyazingatia bila kuhisi kuwa biashara zao zinakwamishwa.
"Utekelezaji na usimamizi wa Sheria ya Huduma za Habari unaonesha ni kwa kiwango gani Serikali inaunga mkono uwekezaji wa vijana katika sekta ya habari. Kazi ya Bodi si kuzuia watu kufanya biashara, bali kuwaelekeza kufuata matakwa ya sheria na kuwahamasisha kuongeza elimu na kukidhi vigezo vinavyotakiwa," alisema Diamond.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa sheria unahitaji busara, maarifa na uwezo wa kuwaelimisha wadau ili waelewe mabadiliko ya taratibu bila kujenga hofu au kuona kuwa wanawekewa vikwazo.
"Kazi hii inahitaji busara na maarifa ya kuwafundisha watu, kuwaelekeza na kuwafanya waelewe taratibu mpya pasipo kuona kwamba wameharibiwa biashara zao. Nimeona Bodi ina timu nzuri inayounga mkono maono ya uongozi wake katika kusimamia sekta hii," alisema Diamond.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula, alimpongeza Diamond kwa uwekezaji wake katika sekta ya habari na kwa Wasafi Media kuendelea kuzingatia matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari.
Alisema JAB itaendelea kushirikiana na wamiliki wa vyombo vya habari na wadau wengine kuhakikisha sheria inatekelezwa kwa njia inayokuza weledi, uwajibikaji na maendeleo ya sekta ya habari, huku ikitoa elimu na ushauri unaowawezesha wadau kutekeleza matakwa ya sheria kwa ufanisi.
Ziara ya Diamond katika Banda la JAB ilikuwa sehemu ya maadhimisho ya JAB Day yaliyofanyika ndani ya Banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, ambapo Bodi imekuwa ikitoa huduma za ithibati, elimu kuhusu Sheria ya Huduma za Habari na ushauri kwa waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari na wananchi.






No comments:
Post a Comment