HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 15, 2026

Wataalamu Wataka Serikali Kuongeza Madaktari wa Magonjwa ya Kinga kwa Watoto

 


Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WATAALAMU wamewahimiza wanafunzi wa tiba na madaktari bingwa wa watoto kujikita katika fani ya Pediatric Rheumatology (Magonjwa ya Mfumo wa Kinga na maungio yanayoathiri watoto) ili kupunguza uhaba mkubwa wa wataalamu katika nchi na barani Afrika kwa ujumla.

Licha ya kuongezeka kwa magonjwa hayo, takwimu zinaonyesha kuwa Afrika yenye zaidi ya watu bilioni 1.4 ina wataalamu wasiozidi 20 wa magonjwa hayo ya watoto (pediatric rheumatologists) katika bara zima, huku Tanzania ikiwa na mtaalamu mmoja tu, hali ambayo wataalam wanaieleza kuwa ya kutia wasiwasi kwa watoto wanaougua magonjwa ya kinga mwilini na ya viungo.

Kimataifa, tafiti zinaonyesha kuwa magonjwa ya rheumatic, ambayo huainishwa kama magonjwa adimu, huathiri watoto kati ya mmoja hadi wanne kwa kila watoto 1,000 duniani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa sita wa magonjwa ya viungo na misuli kwa watoto wa Afrika lililofanyika leo Mei 14, 2026 kwa mfumo wa mseto jijini Dar es Salaam , Profesa Francis Furia kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) alisema uhaba wa wataalamu umesababisha watoto wengi kuchelewa kugundulika na kukosa matibabu kwa wakati, jambo linalozidi kuzorotesha hali zao za kiafya.

Profesa Furia, ambaye ni daktari wa watoto, alisema kuongeza idadi ya wataalamu wa pediatric rheumatology kutaimarisha kwa kiasi kikubwa huduma za afya kwa watoto na kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wengi wanaoathiriwa na magonjwa hayo.

“Kwa sababu ya changamoto hizi, tunaendelea kusisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya wataalamu katika fani hii. Kupitia kongamano hili la sita, tumewapatia mafunzo madaktari wanaoendelea na mafunzo na madaktari wa watoto ili waweze kutambua dalili mapema na kutoa matibabu kwa wakati,” alisema Profesa Furia.

Pia aliipongeza serikali kwa hatua inazochukua katika kuimarisha huduma hizo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Tanzania imeanza kupiga hatua. Uwekezaji mkubwa umefanyika Muhimbili ambapo huduma hizi zinatolewa. Maabara zimeboreshwa na vipimo vingi ambavyo awali vilikuwa vikifanyika nje ya nchi sasa vinafanyika hapa nchini,” alieleza.

Aliongeza kuwa hospitali hiyo imeanzisha kliniki maalum kwa watoto wanaougua magonjwa hayo, ambapo zaidi ya watoto 50 kutoka mikoa mbalimbali wanapata matibabu.

“Hii ni hatua muhimu kuhakikisha watoto hawa wanapata huduma wanazostahili,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Dkt. Gunini Kamba alisema serikali iko tayari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa fursa za elimu, ikiwemo udhamini wa masomo hasa katika fani adimu za tiba.

“Tunahamasisha wote wenye nia na uwezo kujitokeza na kusomea fani hizi maalum ili kusaidia kuboresha huduma za afya nchini,” alisema.

Rais wa Jumuiya ya Madaktari wa Watoto wa Umoja wa Afrika dhidi ya Magonjwa ya Rheumatism (PAFLAR), Dkt. Ayodele Faleye alizitaka serikali za Afrika kusaidia udhamini wa madaktari wa watoto wenye nia ya kujikita katika pediatric rheumatology.

“Kuna uhitaji mkubwa wa kuwazalisha wataalamu zaidi katika fani hii,” alisisitiza.

“Tunahitaji kwa dharura kuimarisha uwezo wa maabara. Katika nchi nyingi za Afrika, sampuli za damu bado hutumwa nje ya bara kwa ajili ya uchunguzi. Hii husababisha kuchelewa kwa matokeo ya uchunguzi na matibabu, ambapo wakati mwingine huchukua siku 7 hadi 10.”

Aliongeza kuwa kuimarishwa kwa maabara za ndani kutasaidia utambuzi wa haraka na kuanza matibabu kwa wakati.

Pia alisema upatikanaji wa dawa muhimu bado ni changamoto kubwa, akieleza kuwa dawa nyingi huagizwa kutoka nje ya Afrika, jambo linalofanya ziwe ghali na wakati mwingine kukosekana.

“Uingiliaji wa serikali ni muhimu kuhakikisha dawa zinapatikana kwa uhakika na kwa bei nafuu,” alisisitiza.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad