HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 27, 2026

MHANDISI JOANES AWATAKA OLCHORONYORI KUWA MABALOZI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

 

Na Mwandishi wetu, Simanjiro
HALMSHAURI ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, baada ya kupata mradi wa mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi (SCALE), wataalamu mbalimbali wamekuwa wakipita maeneo tofauti yatakayonufaika na mpango huo kwa kutoa elimu kwa jamii.


Wananchi wa Kijiji cha Olchoronyori Kata ya Msitu wa Tembo, wamepatiwa elimu endelevu kuhusu mbinu za kuhimili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni mkakati wa kujenga jamii inayostahimili majanga ya kimazingira.

Elimu hiyo imetolewa kupitia Mpango wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (SCALE), kwa kipindi cha miaka mitano. Lengo likiwa ni kuwajengea wananchi uelewa wa namna ya kuzuia na kukabiliana na majanga kama vile ukame wa muda mrefu, mafuriko, milipuko ya magonjwa, pamoja na tishio la njaa.

Akizungumza katika mkutano wa wananchi uliofanyika katika kijiji hicho mwezeshaji wa mafunzo hayo mhandisi Joanes Martine amewataka wananchi kuwa mabalozi wema katika jamii zao kwa kuhakikisha wanasimamia sheria na taratibu za utunzaji wa mazingira.

“Nawasihi mkawe mabalozi katika jamii zenu. Shirikianeni kwa pamoja kufuata kanuni bora za utunzaji wa mazingira ikiwemo upandaji wa miti, kilimo endelevu, na kukomesha kabisa tabia ya ukataji miti ovyo pamoja na uchomaji mkaa,” alisisitiza mhandisi Joanes.

Pia, mwezeshaji huyo amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kuchochea maendeleo kwa kuibua miradi na fursa mpya zitakazovutia uwekezaji zaidi kutoka serikalini, hatua itakayosaidia kukuza uchumi wa jamii hiyo na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, mpango huo unafanyika kwa kuratibiwa na timu ya mabadiliko ya tabianchi kutoka ngazi ya Halmashauri (CCAT) kwa kushirikiana na timu ya mabadiliko ya tabianchi ngazi ya kata (WCAT).

Kata sita za Oljoro namba tano, Shambarai, Msitu wa Tembo, Loiborsoit, Ruvu Remit na Kitwai zinatarajiwa kunufaika na mradi huo wa SCALE.

Mradi huo wa SCALE unatekelezwa katika mikoa 21 ya Tanzania bara katika halmshauri 54 na mikoa mitano ya Zanzibar kwenye Halmashauri 11.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad