HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, May 27, 2026

Kafulila Aitaja PPP Suluhisho la Ufanisi wa Viwanja vya Ndege

 



Na Mwandishi Wetu
URUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP Centre), David Kafulila, amesema mfumo wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ni suluhisho muhimu la kuongeza ufanisi wa viwanja vya ndege, akitolea mfano mafanikio yaliyopatikana katika huduma za Hijja nchini Saudi Arabia.

Kafulila amesema maboresho yaliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Abdulaziz (KAIA) uliopo Jeddah yameonyesha namna uwekezaji kupitia PPP unavyoweza kubadili utoaji wa huduma kwa kiwango kikubwa, hasa kwa mahujaji wanaosafiri kuelekea Makka.

Akitoa salamu za Eid al-Adha kwa Waislamu duniani, Kafulila amesema kabla ya maboresho hayo, mahujaji walikuwa wakitumia kati ya saa sita hadi 10 kukamilisha taratibu mbalimbali za uwanjani, hali iliyokuwa ikisababisha usumbufu mkubwa na ucheleweshaji wa huduma.

Hata hivyo, amesema baada ya utekelezaji wa mradi wa PPP wenye thamani ya dola milioni 249 za Marekani, muda huo umepungua kwa kiasi kikubwa hadi kati ya dakika 45 na saa moja, jambo lililoongeza kasi ya huduma na kurahisisha safari za mahujaji.

“PPP imeongeza ufanisi mkubwa sana. Kabla ya mradi huu, uwanja ulikuwa ukihudumia wastani wa mahujaji milioni moja kwa mwaka, lakini sasa unahudumia kati ya abiria milioni nane hadi tisa kwa mwaka,” amesema Kafulila.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yalitokana na utekelezaji wa mkataba wa miaka 20 kati ya Mamlaka ya Anga ya Saudi Arabia (GACA) na kampuni binafsi ya Hajj and Umrah Terminals Development Company, ukihusisha Saudi Binladin Group pamoja na Aéroports de Paris Management huku Shirika la IFC likiwa mshauri mwelekezi.

Kwa mujibu wa Kafulila, uzoefu huo unapaswa kuwa somo kwa Tanzania katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga kupitia mfumo wa PPP ili kuongeza ufanisi wa viwanja vya ndege, kuboresha huduma kwa wasafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi.

“Tusiogope kuwakaribisha wawekezaji kupitia PPP kwenye viwanja vyetu vya ndege ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuchochea mageuzi ya kiuchumi,” amesema.

Aidha, amesema tathmini ya sekta ya usafiri wa anga duniani ya mwaka 2023 inaonyesha kuwa licha ya viwanja vya ndege vinavyoendeshwa kwa mfumo wa PPP kuwa asilimia 14 pekee duniani, vinahudumia karibu asilimia 40 ya abiria wote duniani.

“PPP na ufanisi ni pacha,” amesema Kafulila huku akiwatakia Waislamu wote Eid Mubarak yenye amani na baraka tele.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad