HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, May 9, 2026

DKT. SAMIA AISISITIZA UTU NA HAKI KWA WAFUNGWA WANAWAKE, AAGIZA MAZINGIRA YA MAREKEBISHO YAZINGATIE UBINADAMU

Na Janeth Raphael MichuziTv 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa kulinda na kuheshimu utu, haki na heshima za wafungwa wanawake, akieleza kuwa licha ya makosa yao ya kisheria, bado wanabaki kuwa binadamu wanaostahili kutendewa kwa staha na kuzingatiwa haki zao msingi.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Mei 9, 2026, wakati akihutubia katika hafla ya kufunga Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi Na. 48 ya mwaka wa masomo 2025/26, iliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT), Ukonga jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesisitiza kuwa wafungwa wanawake wana mahitaji maalum kutokana na maumbile yao na majukumu yao ya kibinadamu, hivyo ni muhimu kwa watendaji wa taasisi za marekebisho kuzingatia tofauti hizo katika utoaji wa huduma na usimamizi wa magereza.

“Wale mnaowasimamia wafungwa wanawake, naomba mhakikishe haki zao, utu wao na heshima yao vinazingatiwa. Ni kweli wamekosea na wanaadhibiwa, lakini bado ni binadamu wenye stahiki zao,” amesema Rais Samia.

Aidha, ameeleza kuwa taasisi za marekebisho zinapaswa kuwa sehemu ya kujenga na kurekebisha tabia za wafungwa badala ya kuwa sehemu ya kuvunja matumaini yao. Amesisitiza umuhimu wa uongozi unaozingatia misingi ya utu, usawa na uadilifu katika usimamizi wa magereza.

Rais Samia pia amehimiza kuimarishwa kwa mifumo ya malezi na mafunzo ndani ya magereza ili kuwawezesha wafungwa kupata ujuzi utakaowasaidia pindi watakapomaliza vifungo vyao, na kurejea katika jamii wakiwa na uwezo wa kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa.

Kauli hiyo imeendelea kuonesha msisitizo wa Serikali katika kuboresha mfumo wa urekebishaji na kuhakikisha magereza yanakuwa sehemu ya mageuzi chanya ya kijamii badala ya adhabu pekee.







































 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad