HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 8, 2026

TRA TANGA YAKUSANYA BILIONI 406.17 KWA MIEZI 9,YAVUKA LENGO KWA ASILIMIA 137

 


Na Oscar Assenga, TANGA
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 406.17 katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, ikilinganishwa na lengo la bilioni 296.3 ukiwa ni ufanisi wa asilimia 137.

Akizungumza kuhusu mafanikio hayo leo Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, Casto John, alisema kuwa matokeo hayo makubwa yametokana na mchango na ushirikiano mzuri wa wadau mbalimbali, ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wakuu wa Wilaya, pamoja na vyombo vingine vya serikali ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ukusanyaji wa kodi unafanyika katika mazingira salama na tulivu.

Aidha, aliwashukuru walipa kodi wote kwa mchango wao mkubwa akisisitiza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya wananchi kujitokeza kwa hiari kulipa kodi zao


Pia alipongeza ushirikiano kutoka kwa vyama vya wafanyabiashara kama JW na TCCIA, pamoja na taasisi za serikali na binafsi ambazo zimekuwa zikifanya kazi kwa pamoja kama timu.

Katika hatua nyingine, Meneja huyo alisisitiza umuhimu wa kipindi cha makadirio ya kodi (Januari hadi Machi) kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi huku akiwashukuru walipa kodi waliojitokeza kukadiriwa na kulipa kodi zao.

Hata hivyo, aliwataka wale ambao bado hawajafika kujitokeza haraka kwani ofisi za TRA ziko wazi kwa huduma hiyo.

Alionya kuwa kutakuwa na zoezi la kuwafuatilia wadaiwa wa kodi, likiwemo ukaguzi wa barabarani kwa magari na wafanyabiashara wasiolipa kodi, hivyo ni vyema wakazingatia sheria mapema.

Kuhusu matumizi ya mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFD), amesema bado kuna changamoto katika baadhi ya maeneo kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kutokutoa hivyo niwatake


Aliwataka wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa risiti kwa kila huduma au bidhaa wanayouza, huku akiwahimiza wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa au kupata huduma.

Pia alibainisha kuwa changamoto zozote zinazohusiana na EFD zinapaswa kuripotiwa ili zipatiwe ufumbuzi.

Akizungumzia suala la magendo, alisema Mkoa wa Tanga unapakana na nchi jirani akionya baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia njia zisizo rasmi kuingiza bidhaa nchini .huku akiwataka kutumia mipaka rasmi ili kuhakikisha bidhaa zinakaguliwa na taasisi husika kama TBS kwa ajili ya kulinda afya za wananchi.

Alisisitiza kuwa magendo yana madhara makubwa kwa uchumi wa nchi, kwani husababisha kukosekana kwa takwimu sahihi za biashara, kupunguza mapato ya serikali, na kuathiri wafanyabiashara halali pamoja na wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad